Chelsea itafurukuta kwa Roma leo?

Mtanzania - - Michezo - LONDON, ENGLAND

TIMU ya Chelsea inaweza kuwa katika wakati mzuri itakapovaana leo na AS Roma kutokana na wapinzani wao hao kukabiliwa na wachezaji majeruhi watatu muhimu wa kikosi cha kwanza.

Timu hizo ambazo zinatarajia kucheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya leo katika Uwanja wa Stadio Olimpico, wiki mbili zilizopita timu hizo zilitoka sare ya kufungana mabao 3-3 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Stamford Bridge.

Katika mchezo huo, mshambuliaji wa Roma, Edin Dzeko, alikuwa nyota wa mchezo baada ya kufunga mabao mawili na kuisaidia timu yake kugawana pointi na wenyeji.

Licha ya Chelsea kupata pointi moja wakiwa nyumbani, bado wana nafasi ya kufuzu hatua ya 16 bora. Endapo Chelsea itaifunga Roma inaweza kufuzu kuingia 16.

Hata hivyo, Atletico Madrid iliyopo kundi moja na timu hizo mbili inaweza kujikuta ikifungasha virago iwapo itapoteza mchezo wake leo dhidi ya Qarabag endapo Roma wakishinda dhidi ya Chelsea.

Beki Bruno Peres ambaye alicheza akitokea benchi katika mchezo dhidi ya Chelsea, atakosekana katika mchezo wa leo baada ya kusumbuliwa kifundo cha mguu pamoja na Gregoire Defrel, hivyo kukosekana kwake kutaondoa ladha iliyokuwapo alipokuwa akicheza sambamba na Diego Perotti eneo la ulinzi.

Chelsea ambao wapo kundi C pia watawashuhudia wapinzani wao hao bila ya beki wao, Rik Karsdorp aliyejiunga AS Roma akitokea Feyenoord.

Roma watalazimika kusubiri vipimo vya awali vya nyota huyo na baadaye kufanyiwa majaribio kama mchezaji huyo ataweza kucheza leo.

Mbali na Chelsea na Roma, timu nyingine zinazotarajia kucheza leo ni pamoja na Bayern Munich watakaosafiri kucheza na Celtic, huku FC Basel wakiwa wenyeji wa CSKA Moscow wakati huo Atletico Madrid wakiwa wenyeji wa Qarabag FK na Olympiacos wakiikaribisha Barcelona.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.