‘Ubinafsi, ushirikiano tatizo Mbao FC’

Mtanzania - - Michezo - Na JENNIFER ULLEMBO -DAR ES SALAAM

KOCHA mkuu wa timu ya Mbao FC, Etienne Ndayiragije, amedai kuwa ushirikiano na ubinafsi unachangia kwa timu yake kukosa matokeo mazuri.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ndayiragije alisema kama wachezaji wake wangefahamu kinachohitajika uwanjani ni ushirikiano, timu hiyo ingekuwa moja ya mfano msimu huu.

Ndayiragije alisema bado wachezaji wake wameonyesha kujijali wenyewe, kila mmoja anaangalia upande wake, huku akiwa amejiwekea malengo ya kuonyesha kiwango chake binafsi badala ya kuungana kwa pamoja.

“Kama wachezaji wangu wangekuwa na ushirikiano tungekuwa mbali hivi sasa, ila hili ni tatizo kubwa, jambo ambalo linachangia washambuliaji wetu kushindwa kuonyesha kiwango bora badala yake tunapoteza nafasi za kufunga mabao.

“Mbao si timu ya kushinda mabao chini ya matano au sita uwanjani, mimi ninachoamini kwenye timu kabla ya kujilinda na kulinda lango lenu mnatakiwa kuhakikisha mnapeleka mashambulizi yenye kuzaa matunda kwa wapinzani ili kujiwekea nafasi nzuri ya kushinda,” alisema Ndayiragije.

Kocha huyo alisema wakati huu wakiwa wanajiandaa na mchezo dhidi ya Njombe Mji, atajitahidi kufanyia marekebisho safu yake ya ushambuliaji kwani imeonekana kukosa umakini.

Timu hiyo iliyoweka kambi ya siku mbili mkoani Iringa kabla ya kuelekea Njombe, itashuka dimbani Jumamosi kuvaana na Njombe Mji katika Uwanja wa Sabasaba.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.