Walimu wanaoikejeli Serikali waonywa

Mtanzania - - Kanda - Na HADIJA OMARY

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), Mkoa wa Lindi, kimewataka walimu wanaotumia mitandao ya kijamii kuisema vibaya Serikali waache tabia hiyo.

Badala yake, walimu hao wametakiwa kuwa watulivu na kuwasilisha malalamiko yao kwa kufuata utaratibu ili yaweze kutatuliwa.

Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Lindi, Mlami Jeba, wakati akitoa ufafanuzi kwa walimu katika mkutano wa CWT, Wilaya ya Nachingwea.

Katika maelezo yake, Jeba alisema kwamba, kauli zinazotolewa na baadhi ya walimu kwamba Serikali inakipuuza chama chao si za kweli kwa kuwa CWT wamekuwa wakikutana mara kwa mara na Serikali kutatua kero mbalimbali zinazowakabili walimu.

“Baada ya Serikali kushirikiana na CWT kufanya uhakiki wa madai ya walimu, ilibainika kiasi kikubwa cha madai yalikuwa na kasoro nyingi.

“Kasoro nyingi zilikuwa zimefanywa makusudi kwa ajili ya kuwanufaisha watu kadhaa na kasoro zingine zilisababishwa na walimu kuchelewa kuwasilisha nyaraka zao.

“Kwa hiyo, baadhi ya walimu ambao wamekuwa wakiitumia mitandao ya kijamii kuisema vibaya Serikali kwa sababu haijawalipa madai yao, waache tabia hiyo kwa sababu madeni yote yatalipwa baada ya uhakiki kukamilika,” alisema Jeba.

Wakati kiongozi huyo akisema hayo, katika taarifa ya CWT, Wilaya ya Nachingwea, ilionyesha Serikali imeshalipa madeni ya Sh milioni 102.06 yakihusisha madeni ya likizo, uhamisho na usafiri wa mizigo kwa wastaafu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.