Tanzania yataka kuwa kinara uzalishaji saruji

Mtanzania - - Biashara Na Uchumi - Na AMINA OMARI

TANZANIA ipo katika mkakati wa kuhakikisha inakuwa kinara wa uzalishaji wa saruji katika nchi zilizoko chini ya Jangwa la Sahara kutokana na uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa viwanda hivyo unaoendelea kwa sasa.

Kutokana na uwekezaji huo mkubwa nchini, viwanda vinatarajiwa kuongeza uzalishaji maradufu kutoka tani milioni 10.8 za sasa hadi kufikia tani milioni 20 kwa mwaka.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tanga hivi karibuni, ameeleza mikakati hiyo ya Serikali katika kufanikisha azma ya sera ya viwanda katika kuchochea uchumi wa nchi.

Amesema kwa hatua hiyo ya uwekezaji inaonyesha ni namna gani Serikali imedhamiria kuwekeza kwenye uchumi wa viwanda ili kuhakikisha lengo la uchumi wa kati linafikiwa mwaka 2025.

Anafafanua kuwa kwa sasa hapa nchini kuna viwanda vya kuzalisha saruji takribani 11 ambavyo vina uwezo wa kuzalisha tani milioni 10.8 wakati hitaji halisi la nchini pekee ni tani milioni 4.7 kwa mwaka.

Anasema kuongezeka kwa uwezo wa uzalishaji wa tani za ziada umelenga katika kuhakikisha wanayateka masoko yaliyoko katika nchi za Afrika pamoja na Arabuni.

“Mikakati yetu ni kuhakikisha tunajikita katika ujenzi wa viwanda vya kuzalishaji bidhaa za saruji, bati na nondo kwa ajili ya masoko ya ndani ya nchi na kuuza nchi za nje.

Mwijage anasema kwa Mkoa wa Tanga unatarajiwa kupata uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha saruji kutoka Kampuni ya Kichina ya Sinoma na Kampuni ya Hengya Cement (T) Ltd.

Waziri Mwijage anasema kampuni hiyo inatarajiwa kuzalisha tani milioni 3 kwa mwaka wakiwa wamelenga kuuza bidhaa yao katika masoko yao makubwa duniani.

Amesema ujenzi wa kiwanda hicho ni fursa kubwa kwa sababu utaenda sambamba na ujenzi wa bomba la mafuta la Hoima Tanga na kwamba saruji ambayo itatengenezwa itapata soko la uhakika.

Amesema licha ya mkoa huo kuwa na viwanda vingine vya saruji, bado mahitaji ya saruji nchini ni makubwa na kwamba ongezeko la viwanda litapaswa lisaidie kushusha bei ya saruji.

“Tunahitaji kuwa na viwanda vingi zaidi ili bei ya mfuko wa saruji ishuke na wananchi wa kawaida waweze kumudu bei na kuweza kununua kwa kwa ajili ya kujenga nyumba za kisasa,” amesema Waziri huyo.

Vile vile anasema kuwa kuendelea kuwepo kwa viwanda vingi katika mkoa huo ni tija kwa nchi, kwani mkoa huo ulikuwa na viwanda vingi kama ilivyo kwa Dar es Salaam na Morogoro, lakini vikafa kutokana na mabadiliko ya teknolojia na kwa vile wenye viwanda hawakuwa tayari kuendana na kasi hiyo ya mabadiliko.

“Wawekezaji wa sasa wako tayari kwenda na teknolojia ya kisasa kwa hiyo Watanzania wawe tayari kuwapokea wawekezaji ili tushirikiane nao kukuza uchumi wetu na Tanzania itoke hapa ilipo na kwenda kwenye uchumi wa kati,” amesema.

Licha ya kuongezeka kwa uzalishaji huo, Mwijage anasema malengo ya Tanzania ni kuhakikisha bidhaa ya saruji inayozalishwa hapa nchini inawafikia wateja kwa haraka na gharama nafuu.

“Kwa sasa Serikali inaendelea kujiimarisha kimiundombinu kwa kufanya upanuzi wa bandari zetu, kurekebisha miundombinu ya reli na barabara ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazozalishwa viwandani,” anasema Waziri huyo.

Kwa upande wake, Ofisa Uzalishaji wa Kiwanda cha Saruji cha Kilimanjaro, Hashim Hafidhi, anasema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tani milioni 1.8 kwa mwaka ambapo kiwanda hicho kimejikita katika uzalishaji wa saruji kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya kujengea pamoja na saruji maalumu kwa ajili ya ujenzi wa barabara, madaraja pamoja na majengo makubwa.

Hata hivyo, anasema kwa sasa soko kuu la bidhaa yao lipo nchini wakati wakiendelea kufanya mazungumzo katika masoko ya nje ya nchi ili waweze kuona namna nzuri ya kuyafikia masoko hayo.

“Tunatarajia kutumia Bahari ya Hindi kusafirisha saruji yetu kwenda Somalia, Kenya na Msumbiji, lakini pia ziko nchi za Sudan, DRC na Uganda ambao wako tayari kuchukua saruji tutakayozalisha.”

Licha ya mafanikio hayo ya uanzishwaji wa viwanda, lakini uingiaji wa saruji kutoka nje kwa njia ya magendo imekuwa ni sugu na ni kilio cha muda kwa wamiliki wa viwanda vya saruji hapa nchini.

Hafidhi anasema changamoto hiyo imekuwa ikiathiri kwa kiasi kikubwa soko lao na kusababisha ushindani kuwa mkubwa sokoni kutokana na saruji ya magendo kuuzwa kwa bei ya chini zaidi kwani hawalipi kodi.

“Serikali tunaomba ione namna bora ya kudhibiti uingiaji wa saruji kutoka nje ya nchi kwani unaathiri soko la ndani kwa kiasi kikubwa na kudidimiza uchumi wa viwanda,” anabainisha Hafidhi.

Kiwanda cha Saruji cha Tanga ni moja ya kiwanda kikongwe cha kuzalisha saruji hapa nchini ambapo kwa upande wao wamegusia changamoto ya miundombinu katika usafirishaji wa bidhaa wanazozalisha.

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Saruji Tanga, Reinhardt Swart, ameishauri Serikali kuboresha miundombinu ya reli na bandari ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

Amesema ili sera ya viwanda iweze kutekelezeka kwa vitendo, Serikali ni vema ingewekeza nguvu nyingi katika uboreshaji wa miundombinu ya bandari na reli ili kurahisisha usafirishaji wa malighafi pamoja na bidhaa.

Amesema wazalishaji wanalazimika kutumia gharama kubwa katika usafirishaji wa mizigo yao kwa kutumia njia ya barabara ambayo ina changamoto nyingi ikiwemo ajali pamoja na uharibifu wa barabara. “Serikali ione umuhimu wa kuboresha bandari zetu kwani mizigo mingi itaweza kupita huko pamoja na reli inaweza kubeba shehena kubwa za mizigo, kama kuna uwezekano Serikali ingepeleka reli katika maeneo ambayo hayana miundombinu hiyo,” amesema Swart.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo amesema katika kuhakikisha wanakabiliana na ushindani wa ujio wa viwanda vya saruji jijini Tanga, watahakikisha wanazalisha bidhaa zao kwa ubora na ufanisi mkubwa. Ujio wa viwanda vipya Mkurugenzi Swart anasema katika fursa ya biashara ya viwanda huwezi kutegemea kiwanda kimoja pekee kwa ajili ya uzalishaji kuweza kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi pekee.

Anasema kuwa kutokana na mapinduzi ya viwanda sambamba na teknolojia kukua, walitegemea uwepo wa ushindani wa kibiashara katika bidhaa hiyo, hivyo wapo tayari kwa ajili ya kuendelea kujiimarisha kiuzalishaji zaidi.

“Hatutishwi na ujio wa viwanda vipya bali tutahakikisha tunalinda ubora wa bidhaa zetu na ziwe zenye viwango madhubuti muda wote,” anaongeza Mkurugenzi huyo.

Kiwanda cha Saruji Mtwara

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.