Mikakati Tanga kufufua mkonge yaendelea

Mtanzania - - Biashara Na Uchumi - Na AMINA OMARI - TANGA

Tanzania tunatumia 2% ya mmea mkonge huku tukitupa 98% wakati mmea unatumika wote kuzalisha vitu vingi. – Salum Shamte

TANZANIA ilikuwa ndiyo nchi pekee barani Afrika kupokea zao la mkonge kutoka Jimbo la Yucatan, nchini Mexico mnamo mwaka 1893 na kupandwa mkoani Tanga enzi za Wajerumani walipotawala.

Hapa nchini Mkoa wa Tanga ndio ulikuwa kinara wa kulima zao hilo kwa wingi kutokana na kuwa na mashamba makubwa ikifuatiwa na Morogoro.

Hadi kufikia mwaka 1964, uzalishaji wa mkonge nchini Tanzania ulikuwa ni tani 235,000 kwa mwaka, hivyo kuifanya Tanzania kuwa ndiyo nchi pekee iliyokuwa ikifanya vizuri katika zao la mkonge barani Afrika.

Kutokana na kilimo hicho, ikawa ndiyo sekta ambayo ilikuwa imeweza kuajiri watu wengi hususani katika maeneo ya mashambani kwa ajili ya kujishughulisha na shughuli za kilimo na hivyo kuongoza uchumi.

Kutokana na kilimo hicho, Mkoa wa Tanga ulikuwa na maendeleo makubwa ya kiuchumi kutokana na faida ya uwepo wa zao hilo pamoja na viwanda vilivyokuwepo enzi hizo.

Bidhaa ya nyuzi pekee ndio ilikuwa ikisafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuuzwa katika masoko ya dunia.

Hata hivyo, ujio wa kamba mbadala za nailoni katika miaka ya 1970 uliweza kuua soko la mkonge kwa kiasi kikubwa hali iliyolazimu kushusha uzalishaji na kufikia tani 32,000 pekee kwa mwaka.

Hali hiyo iliashiria anguko kubwa la zao la mkonge nchini licha ya kuwepo kwa sababu nyinginezo kama mabadiliko na ukuaji wa teknolojia.

Ufufuaji mkonge

Miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na jitihada za makusudi zinazochukuliwa na Serikali pamoja na sekta binafsi katika kulifufua zao hilo kutokana na umuhimu wake.

Salum Shamte ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Katani Limited, anasema kuwa kutokana na jitihada zilizoweza kuanza kuchukuliwa toka mwaka 2005

hadi mwaka jana (2016) zao hilo limeanza kuonyesha mwelekeo wa kufufuka.

Anasema mwaka 2005 Serikali iliweza kupata mapato kiasi cha Sh milioni 140 kutoka mauzo ya kamba (singa) za mkonge nje ya nchi tani 849 huku mwaka 2016 ikipata Sh bilioni 3.6 kutokana na kuuza tani 4,837.

Anasema kuwa mafanikio hayo yanatokana na namna walivyoweza kuhamasisha wananchi hususani wakulima wadogo kuweza kulima mkonge katika maeneo yao.

“Mfumo wa ushindani pamoja na kuhusisha wakulima wadogo kumewezesha kulima zao hilo katika maeneo yao sambamba na kupanda mazao mengine ili kuongeza uzalishaji,” anasema Shamte.

Zaidi ya hekta 8263 za mashamba yao wamefanikiwa kupanda zao hilo huku zikibaki hekta 7,322 ambazo bado hazijapandwa zao hili, lakini zipo kwenye mkakati wa kupandwa.

Anasema zao la mkonge katika masoko ya dunia lina thamani sana kwani ni moja ya zao ambalo unapovuna kila kitu kina thamani kutoka maendeleo ya kiteknolojia yalivyo kwa sasa.

“Sisi Tanzania tunatumia asilimia 2% tu ya mmea wa mkonge wote huku tukitupa asilimia 98% baada ya kuvuna wakati kwa sasa mmea huo unatumika wote katika kuzalisha vitu vingi,” anasema Mkurugenzi huyo.

Anasema kwa mabaki ya zao hilo yanatumika katika kuzalishia bidhaa mbalimbali ikiwemo magari, vigae vya kujengea, chakula cha mifugo pamoja na nishati ya umeme.

Shamte anasema kutokana na mahitaji makubwa ya zao hilo hususani katika nchi za Ulaya na Asia, wamelazimika kuanza kulitilia mkazo ili kuhakikisha wanaliteka soko. “Nyuzi za mkonge kwa nchi za wenzetu zinatengeneza viatu, matofali, mabati na wakati wa kujenga zinatumika ili kudhibiti nyumba isiweze kuungua pale ambapo shoti ya umeme inapotokea.

Anaongeza kuwa moja ya malengo waliyokuwa nayo ni kuhakikisha wanaongeza uzalishaji wa zao hilo hadi kufikia tani milioni 1 kwa mwaka ifikapo mwaka 2040 ili kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.

“Kutokana na upigaji vita wa bidhaa zisizo rafiki wa mazingira kama vile bidhaa za plastiki, mkombozi pekee aliyebaki ni kujikita kuwekeza kwenye ulimaji na uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na mkonge ambazo ni rafiki wa mazingira,” anasema Shamte.

Wameweza kugundua kuwa shina la zao hilo linaweza kutumika kuzalisha sukari pamoja na mvinyo.

“Jitihada zinaendelea kutafuta wawekezaji ambao tutaweza kuingia nao ubia ili tuweze kujenga viwanda vya sukari na mvinjo hapa hapa nchini ili kuongeza fursa za ajira na pato kwa serikali,” alibainisha Mkurugenzi huyo.

Shamte anaiomba Serikali pamoja na taasisi za fedha nchini kuona namna bora ya kuweza kufanya uwekezaji wa zaidi wa kifedha ili sekta hiyo iweze kufanya mapinduzi ya kiuchumi.

Kwani amesema zao hilo lina fursa nyingi za uwekezaji hivyo jitihada zilizoanza kuchukuliwa lazima ziendane na kasi ya uwekezaji huo kidunia ili Tanzania iweze kunufaika.

“Kwa sasa viwanda vingi vya kuzalisha kamba na bidhaa vinahitaji ufufuaji ikiwemo kuwepo kwa mashine za kisasa pamoja na mitaji ili kuongeza uzalishaji,” alisema Shamte.

Mkurugenzi huyo amesema ili dhana ya Tanzania ya viwanda iwe ya vitendo ni wajibu wa taasisi za fedha kupunguza masharti pamoja na riba kubwa ili kuweza kuvisaidia viwanda vya ndani ya nchi kumudu mikopo ya benki.

Naye Meneja Uhusiano wa Kampuni hiyo, Theodora Mtegeta, amesema kwa sasa kampuni hiyo ina jumla ya wakulima wadogo 1,273 ambao wanamiliki zaidi ya hekta 15,590. Anasema kati ya hao mkulima mdogo kabisa anamiliki hekta 6 huku mkulima mkubwa akiwa anamiliki takribani hekta 200 ya mashamba ya zao hilo.

Licha ya shughuli za kilimo kampuni hiyo inamiliki

viwanda vya kuzalisha kamba za katani, kiwanda cha kuzalisha bidhaa zitokanazo na mkonge pamoja na kiwanda cha kuzalisha nishati ya umeme.

“Tunahitaji uwekezaji mkubwa katika kiwanda pekee cha kuzalisha nishati ya umeme inayotokana na mabaki ya mkonge pale Hale kwani sasa tunatekeleza sera ya viwanda na umeme ni muhimu sana,” anasema Meneja huyo.

Ni muhimu kama Serikali itaweza kuingia ubia na sekta binafsi ili kupata mitaji ambayo itawezesha kuongeza uzalishaji.

“Sasa kilimo kinafanywa na wakulima wadogo lakini kama kutakuwa na ubia zao hilo linaweza kulimwa kwa ufanisi na kuongeza uzalishaji wake kwa kiasi kikubwa,” amesema Mtegeta.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.