Ng’ombe 700 wadaiwa kufa kwa ukame

Mtanzania - - Kanda - Na RAPHAEL OKELLO

ZAIDI ya ng’ombe 700 wamekufa katika kijiji na Kata ya Ruabu wilayani Bunda kutokana na kukosa kwa maji na majani ya malisho.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Gerald Kuzenza, alisema walikuwa na ng’ombe 1500 lakini kutokana na kukosekana maji na malisho 700 walikufa.

Alisema hali hiyo ilisababisha bei ya bei ya ng’ombe kushuka hadi Sh 15,000 huku wanunuzi wakisusia kununua mifugo hiyo kutokana na kudhoofika mifugo hiyo.

Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Rick Kaduri alithibitisha kufa kwa mifugo hiyo.

Hata hivyo alisema hana uhakika na idadi inayotajwa na wafugaji hao kama inaweza kufikia 700.

“Ni kweli mifugo imekufa katika halmashauri yetu, lakini idadi hiyo ya mifugo ni kutoka maeneo mbalimbali na siyo kijiji kimoja.

Ninachojua kuna ng’ombe wamekufa Ruabu na wengine kwenye Kijiji cha Guta,” alieleza bila ya kufafanua idadi kamili ya mifugo iliyokufa.

Kaduri alisema tatizo la mifugo kufa ni ukame wa muda mrefu.

Alisema wafugaji waliokuwa na ng’ombe wengi ndiyo walioathirika zaidi hivyo akawakumbusha wafugaji kufuga kisasa waweze kumudu hali ya mabadiliko ya tabianchi.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Kanda ya Ziwa, Mrida Mshota alikiri kuwapo tatizo la mifugo mingi kufa kwa ukame na hasa ng’ombe.

Alisema mikakati imekwisha kuanza ya kukabiliana na tatizo hilo kwa kuanzisha mashamba ya majani kwa ajili ya mifugo yao.

Alisema hatua hiyo siyo ya muda mfupi kwa kuwa watanzania wengi na hasa mikoa ya kanda ya ziwa bado wanafuga ng’ombe wa kienyeji na wana mifugo mingi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.