Naibu waziri awaomba wazee wamlindie jimbo

Mtanzania - - Kanda - Na SAMWEL MWANGA

NAIBU Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, amewaomba wazee wa Wilaya ya Maswa kumuombea na kumlindia jimbo hilo anapokuwa akitimiza majukumu ya taifa kwa sababu wazee hao wanawajua maadui zake. Nyongo ambaye pia ni Mbunge wa Maswa Mashariki, aliteuliwa kuwa naibu waziri wa madini Oktoba 7 mwaka huu. Alitaka aombewe ikizingatiwa wizara hiyo ina changamoto nyingi za ubadhirifu wa mali za umma na viongozi wake kutodumu katika nyadhifa zao.

Nyongo alitoa kauli hiyo alipozungumza na wazee wa mji wa Maswa katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, juzi. Alisema uteuzi huo ni heshima kwake na kwa wazee hao kwa sababu bila wao asingeteuliwa.

Aliwaomba wamlindie jimbo hilo anapokuwa akitimiza majukumu ya taifa kwa sababu wanawafahamu maadui zake.

Naibu waziri alisema wizara ya madini ni miongoni mwa wizara ngumu kutokana na changamoto kubwa hasa katika kipindi hiki ambacho Rais Magufuli anapambana kulinda rasilimali za nchi kuhakikisha zinaleta tija katika kuimarisha uchumi wa nchi.

Aliwataka wazee hao kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) waendelee kupata huduma za matibabu kwa gharama ya chini (Sh 10,000) kwa mwaka.

Katika kuonyesha mfano aliwalipia wazee 234 sehemu ya gharama hiyo ambayo ni Sh milioni 1.17.

Akisoma risala ya wazee hao, Sospeter Japhari, alisema wanamuunga mkono Rais Magufuli kwa juhudi zake za kuleta maendeleo, kulinda raslimali za taifa, mapambano ya ufisadi, madawa ya kulevya, kuondoa wafanyakazi hewa serikalini na kujenga uchumi wa kati kupitia viwanda.

“Sisi wazee wa Wilaya ya Maswa kwa umoja wetu tumeamua kwa pamoja kuungana kuwasilisha pongezi zetu za dhati kwako kutokana na juhudi zako unazozichukua kuwaendeleza watanzania,” alisema Mzee Japhari.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.