KENYATTA AIBUKA NA USHINDI WA ASILIMIA 98

Mtanzania - - Mbele - NAIROBI, KENYA

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), imemtangaza mgombea wa Chama cha Jubilee, Uhuru Kenyatta, kuwa ametetea kiti cha urais baada ya kupata asilimia 98 ya kura halali katika uchaguzi wa marudio wa wiki iliyopita, ambao uligomewa na mpinzani wake mkuu wa Nasa, Raila Odinga.

Tangazo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati bila uwapo wa matokeo kutoka majimbo 25 ya uchaguzi ya eneo la Nyanza, ambayo yalishindwa kupiga kura kutokana na uchaguzi kuvurugwa.

Alisema katika majimbo 266 kati ya 290, Rais Kenyatta alipata kura 7,483,895 zikiwa pungufu ya kura 719,395 kufikia zile 8,203,290 alizopata katika uchaguzi uliofutwa.

Mwitikio wa wapigakura ulikuwa asilimia 42.36 kati ya wapigakura 19,611,423 likiwa anguko la asilimia 38.84.

Chebukati alisema masharti ya kurudia uchaguzi yalifikiwa na kwamba chaguzi za marudio zilikuwa halali, huru na za haki.

Alisema mchakato ulikuwa mgumu kutokana na kwamba ulikuwa wa kwanza barani Afrika, katika Jumuiya ya Madola na wa nne duniani kushuhudia uchaguzi wa urais ukifutwa na kurudiwa.

“NImeridhishwa na namna tulivyoweza kufikia masharti yanayotakiwa kwa kutoa uchaguzi, ambao kwa mtazamo wetu na ninaamini wa waangalizi wa uchaguzi ulikuwa huru, haki na halali,” alisema Chebukati.

Akizungumza mapema jana, Makamu Mwenyekiti wa IEBC, Consolata Nkatha, alisema upigaji kura katika maeneo ambayo haukufanyika hauwezi kuathiri matokeo ya mwisho.

Alisema mchakato wa uhakiki ulikamilika katika majimbo ya uchaguzi 266, ikiwamo la Wakenya waishio nje, ambako uchaguzi ulifanyika na kwamba tume kwa mujibu wa Ibara 55(B)(3) ya Sheria ya Uchaguzi, iliamuru rasmi kutangaza rais mteule.

Alhamisi iliyopita, ulifanyika uchaguzi wa marudio ulioamriwa na Mahakama ya Juu Septemba Mosi baada ya kufuta ushindi wa Rais Kenyatta uliotokana na uchaguzi wa Agosti 8 kwa kile ilichosema haukuwa halali na ulijaa kasoro zilizofanywa na IEBC.

Lakini Odinga alisusia uchaguzi mpya, akitoa masharti ya kufukuzwa kwanza kwa baadhi ya maofisa wa IEBC na kampuni iliyopewa kampuni ya kusambaza vifaa vya uchaguzi.

– PICHA: MTANDAO

KAZI: Wahamiaji wakiwa wamekaa pembeni mwa barabara wakati wakisubiri kuelekea kazini katika Jiji la Misrata, Libya mwishoni mwa wiki iliyopita.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.