Benki yatoa matreka ya bilioni 2/- kwa wakulima wa pamba

Mtanzania - - Kanda - Na MWANDISHI WETU

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB) imetoa matrekta 50 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 2.7 kwa Vyama vya Ushirika 50 vya Msingi vya Masoko (AMCOS) vinavyolima pamba katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kuongeza tija na uzalishajji wa zao hilo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine amesema TADB inalenga kuwawezesha wakulima wa pamba hapa nchini waweze kuongeza tija na uzalishaji kama inavyobainishwa katika Mpango wa Mandeleo ya Kilimo Awamu ya Pili(ASDP-11).

“Matreka ni moja ya nyenzo itakayowawezesha wakulima kuongeza uzalishaji kwa kulima maeneo makubwa zaidi kwa kufuata kanuni bora za kilimo cha pamba tofauti na kutumia jembe la mkono,” alisema Justine

Alisema matrekta ni sehemu ya utekelezaji wa ASDP -11 katika kuhakikisha nyenzo bora za kilimo zinawafikia wakulima na kuchagiza uzalishaji zaidi wa malighafi zitakakazotumika kwenye viwanda na kufanikisha azma ya serikali ya kujenga uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025.

“TADB ndiyo benki yenye dhamana kubwa kwa mkulima hivyo tutaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya kilimo kwa kutoa mikopo kwa wakati, nyenzo za kilimo lengo likiwa kumtoa mkulima katika kutumia jembe la mkono,” alisema Justine

Alisema maeneo mengi nchini bado wakulima wanatumia jembe la mkono linaloendelea kudumaza sekta kwa kufanya kilimo cha mazoea hivyo benki benki imejipanga kuwa mkombozi wa mkulima na kufanya kilimo biashara kupitia huduma mbalimbali tutakazozitoa.

“Tumeanza na wakulima wa pamba kwa kuwapatia matreka kupitia vyama vyao na tutaendelea katika maeneo mengine kuhakikisha mazao yote ya kipaumblele yanatengenezewa mazingira bora ili uzalishaji wake uongezeke,” alisema Justine

Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba, Marco Mtunga alisema kupitia mkopo wa viuadudu uliotolewa msimu uliopita na TADB, ambako uliwanufaisha zaidi ya wakulima 600,000 wa pamba umewezesha kuongeza uzalishaji kufikia tani 221,600 ikiwa ni ongezeko la asilimia 67 ikilinganishwa na tani 133,000 zilizozalishwa msimu wa 2017/18.

“TADB mkombozi wetu wa kweli kwani amefanikisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na kuongeza uzalishaji wa zao la pamba ,” alisema Mtunga

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.