Boti ya mwendo kasi Mwanza-Ukerewe yaja

Mtanzania - - Kanda - Na BENJAMIN MASESE

KAMPUNI ya Songoro Marine Transport Boatyard ya Mwanza imesema inatarajia kuwa na chombo cha usafiri kitakachotumia saa moja kutoka Mwanza kwenda Ukerewe badala ya saa tatu kama ilivyo sasa.

Kampuni hiyo inajihusisha kutengeneza meli, vivuko na boti

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Major Songoro alisema wameamua kuwa na chombo chao cha usafiri kitakachotumia muda mfupi kwenda Ukerewe na sehemu nyingine.

Songoro alisema boti inayojulikana kwa jina la RAFIKI .1 ina uwezo wa kubeba abiria 200 na imegawanyika sehemu mbili za abiria wa kawaida na daraja la juu (VIP) ambako kila abiria anakuwa na kiti cha kisasa.

“Kazi yetu ni ujenzi wa meli, vivuko, vivuko na ukarabati wa vyombo vya majini.

“Shughuli hii tunaifanya kwa kiwango kikubwa na ndiyo maana Serikali tunashirikiana kuhakikisha tunaimarisha ubora na usalama wa raia katika vyombo vya majini.

“Hatujawahi kumiliki meli kubwa ama boti licha ya sisi kuvitengeneza na tumeamua kuanza na boti hii ya kisasa.

“Kama mlivyoiona ilivyojengwa ndani na kuwa na viti vya abiria vizuri tena vya kukaa na kuzunguka hasa VIP, kwa wale waliobahatika kusafiriki kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kwa kutumia boti za Kilimanjaro wanajua raha yake.

“Kwa uwezo wa boti hii, mfano kutoka Mwanza kwenda Ukerewe itatumia saa moja tu, tunataka kuleta maajabu ya kuwaondolea abiria kukaa muda mrefu majini.

“Kwa ratiba tuliyonayo kama tutakamilisha mambo yetu na Serikali nadhani Desemba mwaka huu kitakuwa kinafanya safari na tutaweka wazi wapi kitakuwa kinakwenda na gharama zake,”alisema Songoro.

Hata hivyo alivyoulizwa sababu za kutoshinda zabuni za ujenzi wa meli kubwa zinazotangazwa na Serikali, Songoro alisema uwezo wanao wa kutengeneza chochote kile ambacho kinatakiwa hivyo aliiomba Serikali kuwaamini.

Wakati huo huo, Kivuko cha MV Chato kilichokuwa kikifanyiwa ukarabati katika yadi hiyo kwa gharama ya Sh milioni 61 kimekamilika na kuondoka kuendelea na safari zake huku MV Sengerema inayokarabatiwa kwa Sh milioni 589 ikitarajiwa kufanyiwa maboresho kwa miezi mitatu ili kurejea KigongoBusisi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.