Madereva waanza kukamatwa Tanga

Mtanzania - - Mkoa - Na OSCAR ASSENGA

JESHI la Polisi, Mkoa wa Tanga, kitengo cha usalama barabarani, limeanza kuwakamata madereva ambao wanakwepa kutumia Kituo cha Mabasi cha Kange cha jijini Tanga.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga, Solomoni Mwangamilo, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Alisema kwamba, kitendo cha madereva kutotumia kituo hicho, hakiwezi kufumbiwa macho kwa sababu wanaikosesha mapato Serikali.

“Hadi sasa kutokana na operesheni ambayo tumekuwa tukiifanya, tumeshakamata madereva watatu ambao watafikishwa mahakamani ili waweze kujibu tuhuma wanazokabiliana nazo.

“Hatuwezi kuwafumbia macho watu wanaovunja sheria na kitendo cha kuwakamata madereva hao, kitakuwa ni fundisho kwa wenzao wenye utaratibu wa kuvunja sheria za nchi.

“Kwa ujumla, hatuwezi kukubali Jiji la Tanga likose mapato kutokana na upuuzi wa baadhi ya madereva kwa sababu tupo kwa ajili ya kulinda na kusimamia sheria,” alisema Kamanda Mwangamilo.

Wakati huo huo, aliwataka abiria kufunga mikanda wanapokuwa safarini kwani ipo kwa ajili ya usalama wao.

Kwa mujibu wa Mwangamilo, mikanda inaokoa abiria pindi inapotokea ajali kwani inawasaidia wasiumizwe wakati wa ajali.

“Utakuta mtu anasafiri bila kufunga mkanda, lakini anapomwona askari, anakumbuka kuufunga. Kwa hiyo nawaomba abiria wawe na utaratibu wa kufunga mikanda kwa sababu ipo kwa ajili yao na inawasaidia pindi wanapopata ajali barabarani.

“Pamoja na hayo, abiria wanatakiwa kujua kwamba kutofunga mkanda ni kosa kisheria, hivyo wakikamatwa wanaweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.