Wananchi wakerwa mgogoro wa ardhi

Mtanzania - - Mkoa - Na JANETH MUSHI

WANANCHI katika Kijiji cha Emirete, Kata ya Monduli Juu, wamemwomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kuingilia kati mgogoro baina yao na Kijiji cha Lendikinya.

Wananchi wa vijiji hivyo viwili wanagombea eneo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 530 ambalo awali lilikuwa likitumiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) katika kata hiyo iliyopo wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha.

Wakizungumza jana katika kikao kilichofanyika kijijini hapo, wananchi hao wa Emirete walisema kuwa awali mwaka 2016 walilazimika kumzuia kwa mabango waziri mkuu na kumwomba atatue mgogoro huo ambaye aliagiza idara zinazohusika kuutatua ili wananchi waendelee na shughuli za uzalishaji.

Mmoja wa wananchi hao, Victoria Andrea, alisema kwa kuwa suala hilo limeshindwa kutatuliwa kwa haraka na uongozi wa wilaya, wanaomba viongozi hao wa juu waingilie kati mgogoro huo ili waweze kufikia mwafaka.

“TBL walilima kwa kuingia mkataba na kijiji chetu kwa muda mrefu na wawekezaji wengine ila baadaye kuna baadhi ya viongozi walijigawia maeneo yale na kulima kwa muda mrefu.

“Tumelima mwaka juzi na mwaka jana ila cha kushangaza mwaka huu, Lendikinya walivuka mpaka wa msitu na kuingia shambani kwetu.

“Sisi kama wanawake, tunaomba Waziri Mkuu Majaliwa atusikilize na Lukuvi tunamwomba pia aje atusaidie kutatua mgogoro huu kwa sababu unaweza kusababisha madhara makubwa kwa siku zijazo.”

Akizungumzia madai hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Steven Ulaya, alisema wanautambua mgogoro huo na wameshajaribu kuufanyia kazi ila imeshindikana baada ya baadhi ya wananchi kuwafanyia fujo wataalamu waliokwenda kijijini hapa kuainisha mipaka.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.