Baba aua mama, mtoto kisa chakula

Mtanzania - - Leo Ndani - AMINA OMARI NA SAM BAHARI-TANGA/SHINYANGA

JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga, linamshikilia mkazi wa Pongwe, Petro Sabuni kwa tuhuma za kuwaua mkewe na mwanawe kwa kuwakatakata visu kwa madai ya kunyimwa chakula.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 6, mwaka huu usiku katika eneo la Uroa Kata ya Pongwe.

Alisema mtuhumiwa Sabuni aliporudi kutoka katika matembezi yake alimuomba mkewe amtengee chakula na kujibiwa kuwa chakula kilikuwa kimeisha ndipo alipomchoma kisu.

“Wakati akiendelea kumpiga visu ndipo alipotokea mwanae wa kiume kwa ajili ya kumtemtea mama yake naye alijeruhiwa vibaya,” alisema Kamanda Bukombe.

Alisema kutokana na majeraha waliyoyapata wote walifariki dunia wakati wakikimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Aliwataja marehemu hao kuwa ni Luciana Martine (45) ambaye ni mke wa Sabuni na mtoto wake, Seveme Ndumbo (30).

Kamanda Bukombe alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi dhidi ya mtuhumiwa na utakapokamilika atafikishwa mahakamanikwa hatua za sheria. MWINGINE AUA MKE Wakati huohuo, Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia mwendesha bodaboda mkazi wa Kata ya Ibadakuli mjini Shinyanga, Shyrock Kimaro (48), kwa tuhuma za kumuua mke wake kwa kumpiga na jiwe kubwa kichwani.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Alchelaus Mutalemwa alimtaja mwanamke aliyeuawa kuwa ni Bupe Mwakibibi ambaye alikuwa mfanyakazi wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) Mkoa wa Shinyanga.

Alisema tukio hilo lilitokea Novemba 5, mwaka huu jioni katika Mtaa wa Miti Mirefu Manispaa ya Shinyanga.

Kamanda alisema mtuhumiwa Kimaro anadaiwa kufika nyumbani kwa mkewe huyo na kuanza vurugu.

Alisema kwa mujibu wa walioshuhudia ugomvi huo, Kimaro alikuwa amelewa na walikuwa na ugomvi wa muda mrefu kiasi cha kutengana.

Kamanda alisema siku hiyo mtuhumiwa alifika nyumbani hapo akiwa amelewa na wakazozana hali iliyosababisha kugombana na hatimaye kusababisha mauti ya mwanamke huyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.