Serikali inamiliki shule za sekondari zaidi ya 3,600

Mtanzania - - Mkoa -

SERIKALI inamiliki na kuendesha shule za sekondari,3,634 Tanzania Bara na kati ya hizo shule 3,519 ni za kutwa na 155 ni za bweni.

Hayo yalielezwa bungeni jana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),Joseph Kakunda alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalum,Catherine Ruge (Chadema).

Katika swali lake,Ruge alitaka kujua ni kwa nini Serikali isije na mpango mahususi wa ujenzi wa mabweni kama ilivyofanya kwenye madawati kuwapunguzia wanafunzi hasa wa kike umbali mrefu wa kutembea na kurudi nyumbani.

Akijibu swali hilo,Kakunda alisema Serikali inamiliki na kuendesha shule za sekondari,3,634 Tanzania Bara ambako kati ya hizo shule 3,519 ni za kutwa na 155 ni za bweni.

“Idadi hiyo ikilinganishwa na kata 4,420 inabainisha kuwapo kata ambazo hazina shule za sekondari hivyo zipo changamoto za baadhi ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule kwenye kata za jirani,”alisema.

Alisema Serikali imetumia zaidi ya Sh bilioni 29 kujenga mabweni 298 kwenye shule za sekondari na mabweni 206 kwa shule za msingi. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018-2019,Serikali imepanga kutumia zaidi ya Sh bilioni 15 kujenga mabweni 206 katika shule za sekondari na manne kwa shule za msingi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.