Sethi ahojiwa na Takukuru

Mtanzania - - Habari - Na KULWA MZEE

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwamba tayari wamefanikiwa kumhoji kigogo wa IPTL, Harbinder Sethi kama ambavyo waliomba.

Hayo yalidaiwa jana na Wakili wa Serikali kutoka taasisi hiyo, Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo inatajwa.

“Mheshimiwa Hakimu, upelelezi haujakamilika, mara ya mwisho tuliomba kumchukua maelezo mshtakiwa wa kwanza Sethi, tumefanikiwa kuchukua maelezo yake jana (juzi) tunaendelea na hatua inayofuata,” alidai Swai.

Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 22 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wanaendelea kusota rumande.

Mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni James Rugemalira na kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu.

Mashtaka mengine ni kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha Serikali hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Washtakiwa hao wapo rumande kutokana na kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.