Nida yasajili Watanzania mil. 19

Mtanzania - - Habari - Na CHRISTINA GAULUHANGA

MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), hadi sasa imesajili Watanzania milioni 19.5 na kwamba lengo kuu ni kusajili milioni 22 hadi kufikia Desemba.

Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Nida, Rose Mdame alisema mkakati waliojiwekea ni kuhakikisha wananunua mashine za kisasa ambazo zitasaidia kukamilisha lengo hilo.

Alisema hadi sasa wanaendelea na usajili kupitia mashine ndogo walizonazo kwa kuwa kazi hiyo ni endelevu.

“Usajili wa mkupuo, ule wa mitaa na vijiji umemalizika, kwa sasa tunaendelea na usajili wa kawaida,” alisema Rose.

Alisema kwa mikoa ya Katavi, Rukwa, Kigoma na Kagera bado hawajamaliza usajili kwa sababu ya changamoto ya wageni, ikiwamo kuwa pembezoni.

Rose alisema pia wapo mbioni kuendelea tena na usajili katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga ambayo ina wageni wanaoingia na kutoka kila kukicha.

Alisema hadi kufikia Desemba, wanataka asilimia 86 ya wananchi wawe wamesajiliwa na Nida.

Akizungumza kuhusu maonesho ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba yaliyomalizika Julai 13, mwaka huu, alisema wamefanikiwa kusajili watu 9,340 na mkakati wao ilikuwa ni 10,000.

“Kwa waliotimiza vigezo walipata vitambulisho vyao na kwa wale ambao taarifa zao hazijakamilika, tunaendelea kuwasiliana nao ili watimize masharti na kwa wasio na vigezo hawawezi kupata vitambulisho hivyo,” alisema Rose.

Alisisitiza umuhimu wa vitambulisho hivyo kuwa ni pamoja na kutambulisha uraia kwa na mambo mengine ya kitaifa.

“Vitambulisho hivi pia vinasaidia kuipunguzia gharama Serikali katika masuala mbalimbali ya utambuzi na kutoa huduma za uhakika,” alisema Rose.

PICHA: LOVENESS BERNARD

MKUTANO: Mkurugenzi wa Itifaki Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu kukamatwa kwa waandishi wawili wa Kamati Maalumu ya Kuwalinda Waandishi wa Habari Duniani. Kulia ni ofisa habari wa chama hicho, Tumaini Makene.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.