Wadau wakutana kujadili sheria ya maadili

Mtanzania - - Habari - Na MWANDISHI WETU

WADAU mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi, wamekutana kujadili rasimu ya kanuni za sheria ya maadili namba 13 ya mwaka 1995 kuhusu udhibiti wa mgongano wa masilahi.

Akizungumza katika warsha hiyo iliyofanyika Dar es Salaam jana, Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji mstaafu Harold Nsekela, alisema tangu kutungwa kwa sheria hiyo miaka 23 iliyopita, hazijawahi kutungwa kanuni zinazoshughulikia masuala ya mgongano wa masilahi.

Jaji Nsekela alisema kanuni hizo zikitayarishwa na kuanza kutumika, zitatoa ufafanuzi wa mambo yanayosababisha mgongano wa masilahi na kuweka utaratibu wa kuutatua.

“Katika mazingira haya, hitaji la kuwa na kanuni inayofafanua na kuweka utaratibu wa utekelezaji wa sheria ya maadili ni muhimu kwa sasa ili kuongeza ufanisi na utendaji bora wa taasisi simamizi.

“Mgongano wa masilahi ni tatizo linaloathiri maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Nchi nyingi duniani zinakabiliwa na tatizo hili na madhara yake yanatofautiana kati ya nchi moja na nchi nyingine kwa kutegemeana na ukubwa wa tatizo,” alisema Jaji Nsekela.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alisema ushirikishwaji wa wadau mbalimbali katika kukuza na kusimamia maadili nchini, kutasaidia kukuza uelewa wa pamoja wa mfumo unaoandaliwa kudhibiti mgongano wa masilahi katika sekta ya umma.

“Naamini mnafahamu kwamba masuala mengine ya mgongano wa masilahi yanatokana na viongozi kuwa na majukumu zaidi katika jamii ambayo yanaingiliana na wajibu wao kwa umma.

“Sisi tunafahamu zaidi ni masuala gani yanaweza kusababisha migongano kati ya masilahi ya umma na masilahi binafsi. Hivyo tuisaidie Sekretarieti ya Maadili kwa kuweka mienendo hiyo ili waweze kupendekeza hatua za kuidhibiti hali hiyo,” alisema.

Mgongano wa masilahi ni tatizo linaloathiri maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii -Jaji Nsekela

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.