Wanaokula kwa mama lishe hatarini kuugua kansa

Mtanzania - - Habari - Na UPENDO MOSHA

WATU wanaokula vyakula aina mbalimbali kwa wauza vyakula waitwao mama ntilie, wako katika hatari ya kupata madhara mbalimbali ya kiafya ikiwamo ugonjwa wa saratani kwa kuwa wauza vyakula hao wanatumia mifuko ya plastiki kufunikia vyakula vyao.

Haya yameelezwa juzi na mdau na mwanaharakati wa mazingira mkoani Kilimanjaro, Hanta Fuime, wakati akizungumza na madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, mkoani hapa kuhusu madhara yanayotokana na mifuko ya plastiki pamoja na bidhaa nyingine za plastiki.

“Utakuta mama ntilie wengi wanapika chakula na kisha kukifunika na mifuko ya plastiki maarufu kama malboro ili kiive upesi.

“Hao wanafanya hivyo bila kujua madhara ambayo yatawapata wateja wao na hata wao wenyewe maana na wao pia hula chakula wanachopika.

“Tabia hiyo ya kufunika chakula ili kiive upesi, pia imekuwa ni chanzo cha athari nyingine ambazo ni pamoja na kuathiri mfumo wa uzazi kwa watu hususan wanawake.

“Tabia hii haiko kwa akina mama ntilie tu bali hata majumbani, utakuta kuna watu wanachemsha maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwamo kunywa na kuyahifadhi katika ndoo za plastiki au vyombo vingine vya plastiki.

“Hii ni hatari kwa afya za binadamu, hivyo kila mtu hana budi kuepuka matumizi ya plastiki ya namna hii,” alisema.

Kwa upande wake, Ofisa Afya wa Manispaa ya Moshi, Mgeta Sebastian, alisema tayari halmashauri hiyo imeshaanza kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara za vyakula kama mama ntilie na wengine wanaojihusisha na biashara za namna hiyo kwa lengo la kuokoa maisha ya watu.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi kuepuka au kupunguza matumizi ya mifuko ya plastiki na kuitumia pale tu kunapokuwa na ulazima.

– PICHA: MPIGAPICHA WETU

MKUTANO: Mwenyekiti wa Bodi ya Wakandarasi (CRB), Consolatha Ngimbwa, akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo kwa wakandarasi jijini Arusha juzi. Katikati ni Makamu Mwenyekiti wa CRB, Joseph Tango na Kaimu Mkuu wa Idara ya Utafiti wa CRB, Bhoke Magira.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.