WMA waendelea kukagua mizani

Mtanzania - - Habari - Na MWANDISHI WETU

WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA), wameendelea kutoa elimu pamoja na kuhakiki mizani katika vyama mbalimbali vya ushirika vya msingi Mkoa wa Lindi.

Akizungumza mjini Lindi jana, Meneja wa WMA, Mkoa wa Lindi, Yunior Mbwambo, alisema uhakiki na utoaji wa elimu juu ya mizani hiyo, unafanyika katika wilaya za Nachingwea, Ruangwa na Lindi Vijijini.

Alisema pia kwamba, hadi sasa mizani 128 imeshakaguliwa katika vyama vya msingi 44 na kwamba kazi hiyo inafanywa na ofisi ya WMA, Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na makao makuu.

“Wakati wa zoezi hilo, tunatarajia kutembelea vijiji 340 ambavyo vina jumla ya vyama vya ushirika 150 ambako tutakuwa tukitoa elimu na kufanya kaguzi za kushtukiza kwa wanunuzi wa korosho kwa lengo la kujiridhisha juu ya mizani inayotumika.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa WMA, Stella Kahwa, alisema sheria ya vipimo, sura ya 340, inawataka wakala wa vipimo kuhakiki na kupiga chapa vipimo vyote vinavyotumika katika biashara.

“Wakati wa operesheni yetu, wote watakaobainika kuchezea mizani kwa ajili ya kuwaibia wakulima, adhabu yao ni kuanzia faini ya shilingi laki moja hadi milioni ishirini au kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka mitatu baada ya mtuhumiwa kufikishwa mahakamani na kupatikana na hatia.

“Wakati huo huo, ieleweke kwamba hadi sasa katika zoezi linaloendelea mkoani Lindi, mizani sita inayotumika katika ununuzi wa korosho, imeonekana kuwa na kasoro na wahusika wameshatozwa faini ya shilingi milioni nne. “Pamoja na hayo, tutaendelea kutoa elimu kwa wakulima na wafanyabiashara ili wajue thamani ya kuuza kwa kutumia mizani iliyohakikiwa na wakala wa vipimo na pia waelewe madhara ya kutumia mizani ambayo haijahakikiwa,” alisema Kahwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.