Wachezaji Taekwondo watakiwa kushiriki mashindano

Mtanzania - - Michezo - Na GLORY MLAY

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Taekwondo Tanzania (TTF), Shija Shija, amewataka walimu wa mchezo huo kuhakikisha wanawapeleka wachezaji kwenye mashindano, pale wanapohitajika kufanya hivyo kwa mujibu wa katiba.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Shija alisema katika mashindano mengi yanayofanyika, mahudhurio yamekuwa hafifu.

Alisema mfano mdogo ni kwenye mashindano ya Nanenane, yaliyofanyika mkoani Arusha hivi karibuni, ambako idadi ya washiriki ilikuwa hairidhishi.

Alisema mashindano hayo yalivikutanisha vilabu mbalimbali kutoka Kenya na wenyeji Tanzania, ambapo jumla ya timu kumi ziliweza kushiriki.

“Taekwondo ni mchezo ambao wachezaji wake lazima wapigane mara kwa mara ili kutoa woga na kuongeza ujuzi, si mchezo wa kuchezea kwenye luninga au kwenye vitabu kama ilivyo baadhi ya michezo, kutowapeleka wachezaji kwenye mapambano ni kuwanyima haki yao ya kikatiba.

Katibu huyo alivipongeza vilabu vyote vilivyoweza kujitokeza kupambana na timu kutoka Kenya na kufanikiwa kubakisha ushindi nyumbani.

“Hii ni dalili nzuri kwa timu zetu, wenzetu Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi wao Taekwondo ni ajira, tofauti na hapa kwetu ambako mchezo huo ni burudani kwa mchezaji mwenyewe,” alisema Shija.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.