SBL yatekeleza ahadi kwa wanariadha

Mtanzania - - Michezo - Na MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya vinywaji baridi, SBL Tanzania Limited, imejitosa kuwadhamini wanariadha wawili, Samson Lyimo na Grolia Makula kwa ajili ya kushiriki mbio za Beirut Marathon zitakazofanyika nchini Lebanon.

Wanariadha hao zao la Dar Rotary Marathon yaliyofanyika hivi karibuni, watakuwa wawakilishi wa Tanzania katika mbio hizo, zinazotazamiwa kuwa za aina yake.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Meneja Mafunzo na Uwezeshaji wa SBC, Rashid Chenje, alisema wana imani wanariadha hao watakuwa wawakikishi wazuri.

Alisema kwa sasa wameanza na wanariadha hao wawili, lakini wanaweza kuongeza idadi hapo baadaye kwa kuwa huo ni mwanzo baada ya kutambua thamani ya mchezo wa riadha hapa nchini.

“Sisi SBC tumefarijika kudhamini hawa wachezaji, tuna imani nao hawatatuangusha, kwani sisi wasambazaji wa vinywaji baridi jamii ya Pepsi, Mirinda, 7up, Mountain Dew na Evervess, tunatambua thamani kubwa ambayo Watanzania wametupatia, hivyo ndio maana tumeamua kuanza na hawa,” alisema.

Aliongeza kuwa SBC itawagharamia wanariadha hao tiketi za ndege za kwenda na kurudi, viza, chakula, malazi na bima ya safari kwa siku watakazokuwepo nchini Lebanon.

“Hii ni fursa nzuri kwa wanariadha wetu kupeperusha bendera ya Tanzania katika mbio hizo za kimataifa, pia nawashukuru RT kwa ushirikiano wao mpaka kufanikiwa kukamilisha hili na pia tunawapongeza viongozi wa Dar Rotary Marathon kwa kuwaibua nyota hawa,” alisema.

Naye Gloria aliwaomba Watanzania kumwombea dua ili akawe mwakilishi mzuri na kurejea na medali na kuitangaza vyema Tanzania katika uwakilishi wake.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.