SIRI YA CHIRWA KUTUA AZAM HADHARANI

Mtanzania - - Michezo - Na THERESIA GASPER

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Hans van der Pluijm, ametaja sababu za kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Obrey Chirwa, kuwa ni mchezaji mpambanaji na asiyekata tamaa akiwa ndani ya 18.

Klabu ya Azam FC jana ilimtambulisha rasmi Chirwa kuwa mchezaji wake baada ya kumsajili kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Chirwa ataanza kuichezea Azam baada ya kufungwa kwa dirisha dogo, ambalo litafunguliwa Novemba 15 na kumalizika Desemba 15.

Chirwa alipata kuichezea Yanga kwa misimu miwili, 2016/17 na 2017/18 kabla ya kutimkia zake Misri na kujiunga na klabu ya Ismailia ya Misri ambayo hivi karibuni alivunja nayo mkataba.

Chirwa alitaja sababu ya kuvunja mkataba na klabu hiyo kuwa ni kutokana na kukiukwa kwa makubaliano, ambapo aliishutumu Ismailia kwa kutomlipa stahiki zake.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akimtambulisha Chirwa, Pluijm, alisema anamfahamu Chirwa kwa kuwa aliwahi kufanya naye kazi Yanga kuwa ni mpambanaji asiyekata tamaa.

“Binafsi namfahamu Chirwa, kwani nilishafanya naye kazi, naamini ujio wake utasaidia timu kupata matokeo kwa kushirikiana na wenzake,” alisema.

Upande wake Chirwa alisema anafahamu mahitaji ya Azam FC ni kutwaa ubingwa, hivyo atahakikisha anapambana ili kutimiza matarajio ya mabosi wake hao wapya.

“Nitahakikisha nafunga mabao mengi kadiri nitakapopata nafasi ya kucheza, lakini vile vile nitahakikisha nazifunga Simba na Yanga pale nitakapokutana nao,” alisema.

Wakati huo huo, Ofisa Habari wa Azam, Jafar Idd, alisema wamemsajili Chirwa kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine pale atakapofanya vizuri na kuwaridhisha mabosi wa klabu hiyo.

“Tumemsajili Chirwa kwa mkataba mmoja, kuna kipengele cha kuongeza pale tutakapokubaliana, lakini tutaendelea na zoezi hili la usajili kwa wachezaji wengine pale tutakapokamilisha tutaweka wazi,” alisema.

Katika hatua nyingine, Meneja wa timu hiyo, Philiph Alando, alisema wana mpango wa kumtoa kwa mkopo mchezaji wao, Wazir Junior, ili kumpa fursa ya kucheza mara kwa mara na kulinda kiwango chake.

“Kuna timu kama nne ambazo zinamhitaji ikiwemo Biashara United, Mbao FC, KMC lakini tuna mchezaji wetu anacheza KMC, hivyo hatuwezi kumpeleka huko, tutaangalia kule ambako ataenda kucheza,” alisema.

Chirwa ataanza kuichezea Azam baada ya kufungwa kwa dirisha dogo, ambalo litafunguliwa Novemba 15 na kumalizika Desemba 15.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.