Zungu: Kodi imewakimbiza wafanyabiashara

Mtanzania - - Mbele - Na FREDY AZZAH

MBUNGE wa Ilala, Mussa Zungu (CCM) amesema wafanyabiashara wamekimbia nchini kutokana na kukosekana kwa mazingira rafiki katika masuala ya kodi na ushuru.

Zungu alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akichangia Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2019/20.

Alisema biashara katika maeneo ya bandari na mengine si rafiki kwa wasafirishaji na waingizaji wa bidhaa nchini.

Zungu alisema gharama ya kuingiza kontena la futi 20 katika bandari ya Kenya ni Dola za Marekani 80 ambayo wamepunguza kutoka Dola 103. Alisema kwa Tanzania kontena lenye ukubwa huo gharama zake ni Dola za Marekani 170, hivyo ni vigumu kwa waingizaji wa bidhaa kuvutiwa kuitumia.

Alisema katika Bandari ya Dar es Salaam inayotegemewa kwa usafirishaji ni Dola za Marekani 100, lakini Kenya ni dola 60.

Zungu alisema hali hiyo inafanya watu wengi kuhamia katika bandari yenye unafuu.

“Namwomba waziri aendelee kuchagua ushauri wa namna gani anaweza kupunguza ‘tariff’ na ‘importation’ ziwe rafiki kwa wafanyabiashara,” alisema Zungu. Aliitaka pia Serikali kutazama Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwani mwanzo ilikuwa asilimia 20, ikashuka na kuwa 18 na lengo ilikuwa ni kuendelea kuipunguza. Kuhusu sukari ya viwandani, Zungu alisema fedha ambazo wafanyabiashara wanaidai Serikali ni zaidi ya Sh bilioni 45.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.