Sterling aomba radhi kwa kujiangusha

Mtanzania - - Habari - MANCHESTER, ENGLAND

MSHAMBULIAJI wa pembeni wa timu ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini England, Manchester City, Raheem Sterling, amemwomba radhi Mwamuzi Viktor Kassai kwa kujiangusha katika eneo la penalti, juzi kwenye mchezo dhidi ya Shakhtar Donetsk.

Katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya makundi, Manchester City iliibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya wapinzani hao, lakini moja ya bao ni mkwaju wa penalti iliyotokana na Sterling kudaiwa kuchezewa vibaya katika eneo hilo la hatari.

Mchezaji huyo aliweza kuingia kwenye eneo la hatari na hatimaye kupiga chini wakati anataka kufunga bao, kisha kuanguka, jambo ambalo lilimfanya mwamuzi wa mchezo huo, Kassai kuamini kuwa mchezaji huyo amechezewa vibaya na beki wa Donetsk, Mykola Matviyenko.

Hata hivyo, baada ya kuonesha marudio ya tukio hilo, ni wazi kwamba Sterling wala hakuguswa na mchezaji huyo, lakini baada ya kumalizika kwa mchezo huo alimuomba radhi mwamuzi huyo raia wa nchini Hungary.

“Nilikuwa na lengo la kuuchota mpira, lakini nikajikuta naanguka chini na sijui nini kilitokea,” aliieleza BT Sport.

“Ni kweli sikuhisi kama kuna mtu amenigusa, ila ninaamini nilichimba chini na kuanguka, hivyo natumia nafasi hii kwa ajili ya kumuomba radhi mwamuzi wa mchezo huo.”

Hata hivyo, Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, ameweka wazi kwamba, haikuwa penalti, “Tumejiridhisha haikuwa penalti, Raheem alitakiwa kumwambia mwamuzi mapema, hatutaki kufunga mabao ya aina ile,” alisema kocha huyo.

Kwa upande mwingine nyota wa Mancheter City, Gabriel Jesus, aliondoka na mpira baada ya kufunga mabao matatu peke yake, huku mabao mengine yakifungwa na Sterling, Riyad Mahrez na David Silva.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.