Geita kuwa kitovu cha utalii nchini

Mtanzania - - Habari - Na SELEMAN JUMA

SERIKALI ya Mkoa wa Geita imesema iko tayari kushirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT) kuhakikisha mkoa huo unakuwa kitovu cha utalii nchini.

Hayo yalisemwa jijini hapa jana na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Josephat Maganga katika mkutuno uliowakutanisha viongozi waandamizi wa Mkoa wa Geita, wahadhiri wa chuo hicho na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel, mkuu huyo wa wilaya alisema wana shauku kuona wanapiga hatua kimaendeleo kwa kuwa kila kitu wanacho.

“Uongozi wa Mkoa wa Geita una shauku kuona unapiga hatua kimaendeleo kwa kuwa kila kitu tunacho na kazi yetu sisi viongozi ni kutafuta wataalamu wa nyanja mbalimbali watakaosaidia kubuni na kuratibu mradi huu mkubwa wa kuifanya Geita kuwa kituo adimu cha vivutio vya utalii nchini,” alisema Maganga.

Wazo la kuifanya Geita kuwa kituo cha utalii nchini, lilitolewa na mkuu wa mkoa huo na kupanga kuwatumia wataalamu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuhakikisha wazo hilo linafanikiwa.

Naye Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Thereza Mgobi akiwasilisha mada katika mkutuno huo alisema Geita ni miongoni mwa mikoa yenye vivutio adimu vya utalii nchini kutokana na uwepo wa madini, Ziwa Victoria, misitu, Hifadhi ya Taifa ya Lubondo, utamaduni wa Wasukuma na hali nzuri ya hewa.

“Pamoja na uwepo wa vivutio mbalimbali mkoani humo, uwanja wa ndege wa kimataifa uliopo mjini Chato pia utasaidia kwa kiwango kikubwa kuhamasisha sekta ya utalii na hivyo kukuza uchumi wa nchi kutokana na mapato yatakayopatikana.

“Ni ukweli usiopingika kuwa Mkoa wa Geita una fursa nyingi za utalii na cha msingi ni kutengeneza mazingira rafiki ikiwa ni pamoja na uwepo wa hoteli, barabara nzuri, huduma ya maji na umeme,” alisema Mgobi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.