‘Trafiki walarushwa wachukuliwe hatua’

Mtanzania - - Kanda - Na BENJAMIN MASESE

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mwanza kimeishauri serikali kuchukua hatua za haraka kukomesha rushwa za barabarani na kuboresha vivuko ndani ya Ziwa Victoria kuepuka maafa kama ya MV. Nyerere.

Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Mwanza, Saimon Mangelepa alikuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mwanza kilichojumuisha wakuu wote wa idara za serikali.

Alisema wao ndiyo waliopewa dhamana na wananchi hivyo wamebaini baadhi ya maeneo yanahitaji utekelezaji wa haraka.

Mangelepa alisema katika sekta ya usafirishaji kuna haja ya kuboresha vivuko vilivyo ndani ya Ziwa Viktoria kwa kuvifanyia ukaguzi wa mara kwa mara na hata kununuliwa kipya.

Alitoa mfano wa kivuko cha MV Nkome kinachofanya safari zake kati ya Nkome na Nyakarilo Wilaya ya Sengerema kuwa ni kibovu.

“Hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa pale Nkome, kile kivuko cha Nyakarilo-Nkome kinatia shaka na wananchi wanakilalamikia.

“Hivyo hatuhitaji tena vilio tunaiomba Serikali kufanya linalowezekana kuboresha huduma pale yale yaliyotokea Ukerewe yasije kujirudia.

“Kwa upande huo huo wa usafirishaji tunapata malalamiko kutoka kwa wananchi kusumbuliwa na askari wa barabarani ‘trafiki’ kwa kuomba rushwa madereva wanapopatikana na kosa.

“Suala hili limekuwa sugu sana hivyo tunaomba jeshi la polisi likae na vijana wake kuona namna ya kuwakanya kuacha vitendo hivi kwani vinachafua utawala wa awamu ya tano.

“Vile vile ndani ya mitatu ya Rais Dk. John Magufuli amefanya mambo makubwa na kwa muda uliibaki tunaomba Serikali iweze kutenga fedha za kuboresha miundombinu ya barabara za wilayani na nyingine za Jiji la Mwanza kwa sababu nazo ni kero,”alisema.

Mangelepa alisema kamati kuu ya CCM mkoa wa Mwanza imebaini baadhi ya miradi iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi kujenga maboma katika sekta ya elimu, afya na miradi mingine ya jamii imeshindwa kumaliziwa na Serikali kama ilivyoelekeza kitendo kinachowakatisha tama wananchi kuchangia tena.

Alisema kuna maboma katika shule za msingi, sekondari, vituo vya afya na mengine yameshindwa kuezekwa kutokana na Serikali kutotenga fedha.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.