Waziri Mabula awataka wataalamu wasimchonganishe na wananchi

Mtanzania - - Kanda - Na PETER FABIAN

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, amewaonya baadhi ya watumishi wa halmashauri idara ya ardhi na mipango miji kuacha kumchonganisha na wananchi katika mitaa ya kata 19 za Jimbo la Ilemela wanapokwenda kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

Mabula ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo alikuwa akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Ilemela juzi.

Aliwataka wataalamu hao kuacha tabia ta kumchonganisha na wananchi wanapokwenda kudhibiti ujenzi holela katika maeneo mbalimbali ya mitaa za kata zote za manispaa hiyo.

Naibu Waziri aliwataka wataalamu hao kubadilika na kuweka siasa pembeni wakati wa kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria ikiwamo kutoa elimu kwa wananchi katika upimaji shirikishi na utaratibu wa kupata hati za viwanja.

Alisema wanapaswa kufuata utaratibu wa ujenzi wa mipango miji kwa mujibu wa sheria badala ya kudai kutekeleza maelekezo ya Naibu Waziri.

“Wataalamu na watendaji fuateni sheria kwa kutekeleza majukumu bila kuwadanganya wananchi na mtoe elimu kabla ya kutekeleza sheria hizo.

“Wanaotumia majina ya viongozi ni udhaifu na lengo ni kutuchonganisha na wananchi bila sababu ni vema tukajirekebisha na kufuata sheria,”alisema.

Mbunge aliipongeza halmashauri hiyo kushika nafasi ya kwanza kwa mkoa katika matokeo ya darasa la saba.

Aliwataka madiwani kuona namna ya kuwapatia motisha wakuu wa idara ya elimu na walimu wakuu wa shule zilizofanya vema katika wilaya hiyo.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Daniel Batale aliwasilisha taarifa manispaa hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi John Wanga kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2018/2019.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.