Wakandarasi wazawa watakiwa kuchangamkia miradi mikubwa

Mtanzania - - Habari - Na MWANDISHI WETU

Tuungane kutafuta hizo zabuni, zabuni zimetangazwa lakini nasikia hakuna kampuni ya Tanzania ambayo imeomba– Consolata Ngimbwa

BODI ya Wakandarasi Tanzania (CRB), imewataka wakandarasi wazalendo kuchangamkia fursa katika miradi mikubwa ya ujenzi inayoendelea badala ya kuwaachia wageni peke yao huku wao kubaki wakiendelea kulalamika.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na Mwenyekiti wa CRB, Consolata Ngimbwa, wakati akifungua mafunzo maalumu ya siku tatu ya wakandarasi zaidi ya 80 kutoka mikoa mbalimbali kuhusu maandalizi ya zabuni na masuala mengine yanayohitajika kufanyika kabla ya mkataba wa ujenzi.

“Tujitahidi kutafuta zabuni katika miradi mingi inayotekelezwa sasa hivi nchini kama ile ya ujenzi wa kituo cha umeme wa maji wa Stiegler’s Gorge, ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga na mingine,” alisema.

Akitoa mfano wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga, Consolata, aliwataka wakandarasi kuungana na kuomba zabuni zinazotangazwa.

“Tuungane kutafuta hizo zabuni, zabuni zimetangazwa lakini nasikia hakuna kampuni ya Tanzania ambayo imeomba, tusije kushangaa miradi yote inashikwa na Waganda peke yao,” alisema.

Kuhusu mradi wa Stiegler’s Gorge, alisema amesikia mkandarasi aliyepatikana ni kutoka Misri lakini wa hapa nchini wanaweza kuangalia fursa za kushirikiana naye kwa kuwa hawezi kufanya kila kitu peke yake.

“Tujifunze huyo mkandarasi anafanya nini, tusikae tu na kulalamika,” alisema.

Kwa upande wa miradi ya maji ya Serikali, alisema kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa viongozi kuwa utekelezaji wake ama unachelewa au maji hayatoki baada ya ujenzi na akataka kupata maoni yao.

“Nini kilichopo katika miradi hiyo, wakipita viongozi utasikia mkandarasi wa maji kapelekwa Takukuru, sasa hivi wapo baadhi ya wakandarasi wanaogopa hata kuchukua nyaraka za zabuni,” alisema.

Akitoa uzoefu wa tatizo hilo, Mkandarasi Theophillus Kahigwa, kutoka Arusha alisema kumekuwa na siasa nyingi katika utekelezaji wa miradi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.