Yanga yaziundia mkakati pointi sita

Mtanzania - - Michezo - Na MOHAMED KASSARA

BAADA ya Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) kupanga tarehe ya viporo viwili vya Yanga, benchi la ufundi la timu ya Yanga limekutana na kupanga mikakati kabambe itakayowawezesha kuvuna pointi zote sita.

Yanga ina michezo miwili ya viporo dhidi ya timu za Kagera Sugar ya Bukoba na Mwadui ya Shinyanga.

Kwa kujibu wa TPLB, Yanga itashuka dimbani Novemba 22 kuivaa Mwadui FC, Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, kabla ya kushuka tena dimbani Novemba 25 kuikabili Kagera Sugar, Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Katika kuhakikisha wanakusanya pointi hizo, benchi la ufundi la Yanga, lililo chini ya kocha Mwinyi Zahera, limeomba mechi mbili za kirafiki wakati huu wa mapumziko ya kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Zahera anataka mchezo mmoja wa kimataifa na mwingine na timu ya ndani.

Tayari miamba hiyo ya Jangwani imeanza mawasiliano na timu moja kali kutoka Malawi, ambapo kama mambo yataenda sawa, itajipima nayo Jumanne ijayo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Klabu hiyo pia imepokea mwaliko kutoka timu ya Namungo FC ya Lindi, inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Mchezo kati ya Yanga na Namungo utapigwa Novemba 18, Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.

Baada ya mchezo huo, kikosi cha Yanga kitarejea Dar es Salaam kabla ya kwenda Kanda ya Ziwa kuzifuata Mwadui na Kagera Sugar.

Mratibu wa Yanga, Hafidh Salehe, ameliambia MTANZANIA kuwa michezo hiyo ni muhimu kwa kikosi chao, kwani itasaidia kuwaweka sawa wachezaji wao kabla ya kuingia katika vita ya kuwania pointi sita ugenini.

“Ni kweli tupo katika hatua nzuri ya mazungumzo na kuileta timu hiyo ya Malawi.

“Hatuwezi kuiweka wazi kwa sasa kwa kuwa taratibu bado hazijakamilika, benchi la ufundi limependekeza michezo miwili ya kirafiki ili kuwaandaa vijana kipindi hiki cha mapumziko,” alisema Sahele.

“Kama tutafanikiwa kucheza michezo hiyo, itatusaidia kuwajenga wachezaji wetu kisaikolojia, kama unavyojua hatukupata matokeo mazuri sana katika mchezo uliopita na tunakwenda Kanda ya Ziwa ambako ni ngumu kupata pointi tatu, lakini kwa mikakati hii tuliyoiweka tunaamini tutafanikiwa.”

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.