SUMATRA waagizwa kuwabana madereva, wamiliki wazembe

MZALENDO - - HABARI/ TANGAZO - NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) kutoa adhabu kali kwa wamiliki wa vyombo vya usafirishaji na madereva wazembe wanaosababisha ajali za barabarani.

Wito huo aliutoa wakati wa ukaguzi wa utendaji kazi kwa wafanyakazi wa taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo na miundondombinu ya barabara, bandari, mawasiliano na Kiwanja cha Ndege cha Kikwetu mkoani Lindi.

Profesa Mbarawa alisema ongezekolaajalizinazosababisha vifo kutokana na uzembe wa madereva kutofuata sheria na alama zinazowekwa barabarani zidhibitiwe ili kuokoa maisha ya Watanzania na nguvu kazi ya taifa.

“Nataka kuona wamiliki wa vyombo vya usafiri na madereva wazembe wanaposabisha ajali na kuua watu wanafutiwa leseni zao, vilevile nawataka mfikirie kwanini Watanzania wengi wanaendelea kufa kwa ajali za barabarani ili muweze kutafuta ufumbuzi wa namna ya kudhibiti ajali hizo,” alisisitiza Profesa Mbarawa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa alimuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Mhandisi George Sambali kukamilisha kazi ya kupima eneo la kiwanja cha Kikwetu ili kupata hati miliki na kudhibiti uvamizi wa kiwanja hicho.

“Kama kiwanja hiki hakitapimwa watu watavamia eneo la kiwanja na serikali italazimika kuingia gharama za kulipa fidia, hivyo kuchelewesha maendeleo ya uwanja huo”, alisema.

Aliongeza kuwa serikali iko kwenye hatua za mwisho za kutafuta fedha kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ili kuimarisha miundombinu ya kiwanja hicho na kuongeza chachu ya maendeleo mkoani humo.

Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Kikwetu mkoani Lindi, Boniface Njanda, alimwakikishia Waziri Profesa Mbarawa kuwa mamlaka itafanya tathmini ya kiwanja hicho kabla ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.

PROFESA Makame Mbarawa

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.