Waziri Kairuki awashukia watendaji utumishi wa umma

MZALENDO - - HABARI - NA LATIFA GANZEL MOROGORO

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, amewataka watumishi waliopewa dhamana ya kusimamia watumishi wenzao kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na endapo watatiliwa shaka na kulalamikiwa watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Waziri huyo alisema hayo wakati akiongea na viongozi na watumishi wa umma wa Mkoa wa Morogoro kwa lengo la kusikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi.

Alisema wapo watumishi waliopewa dhamana ya kuwa viongozi wa wenzao, lakini wamekua wakijigeuza kuwa miungu watu na kushindwa kusikiliza matatizo au kero za watumishi wenzao na kwamba kuanzia sasa atakayetiliwa shaka, serikali haitaona haya kumchukulia hatua za kinidhamu ikiwa pamoja na kusimamisha mshahara wake. Kairuki

Waziri Kairuki alisema kitendo cha kutosikiliza wateja wao wa ndani ambao ni watumishi wenzao kinachangia kushuka kwa ufanisi kwa watumishi hao, hivyo wananchi kushindwa kupata huduma bora kutoka kwa mtumishi huyo.

Alisema kuanzia sasa serikali itapeleka timu ya wakaguzi katika kila wilaya kwa ajili ya kuchunguza na kusikiliza kero kutoka kwa watumishi wa kawaida na ikibainika wamekuwa wakilalamikiwa, watumishi hao waliopewa dhamana watachukuliwa hatua ikiwemo kushushwa vyeo.

Waziri huyo alisema watumishi hao wamekuwa na wakipeleka malalamiko yao katika ngazi za juu kutokana na waliopewa dhamana kushindwa kutenga muda wa kuwasikiliza kwa ajili ya kutatua kero zao.

Alisema wapo watumishi wenye matatizo ya kutopandishwa vyeo, mishahara kulimbikiziwa malipo miongoni mwao wakipeleka matatizo hayo kwa wakuu wao wa idara wamekua wakiombwa rushwa ya ngono au rushwa ya pesa hivyo kuanzia sasa atakayebainika atachukuwa hatua kali ikiwemo kufukuzwa kazi.

Awali, akimkaribisha waziri huyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe Stephen Kebwe, alisema tayari ameshapita katika halmashauri zote Morogoro na kuongea na watumishi ili kuelezea azma ya serikali ya ‘Hapa Kazi Tu’ na kuwaonya watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na utumishi wa umma.

ANGELLA

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.