Waziri aonya mashirika usambazaji vilainishi

MZALENDO - - HABARI - NA ANGELA SEBASTIAN, BUKOBA

SERIKALI imepiga marufuku mashirika na taasisi mbalimbali kuacha kutoa misaada ya mafuta maalum (vilainishi) kwa watu wanaofanya mapenzi ya jinsia moja. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, aliyasema hayo juzi wakati akizindua jengo la wodi ya wazazi lililojengwa kwa ufadhili wa Shirika la Jhpiego, kwenye Hospitali ya Mkoa wa Kagera.

Ummy alisema mashirika au taasisi zitakazotaka kutoa huduma za kupiga vita maambukizi ya ukimwi, kabla ya kuwafikia walengwa waanzie kwa wakuu wa mikoa husika na kutoa maelezo ya kina ni kitu gani wanaenda kufanya kwa jamii.

“Serikali na viongozi wa dini kila siku wanapiga vita masuala ya ushoga na ukahaba, lakini kuna baadhi ya mashirika yanahamasisha ushoga kwa kutumia mbinu za kutusaidia, hivi tunajenga taifa gani la baadaye linalokiuka utamaduni wake,” alihoji.

Alisema serikali ya awamu ya tano haiwezi kulea masuala ya mapenzi ya jinsia moja (ushoga) na wala haitayapa nafasi mashirika yanayohamasisha mapenzi ya jinsia moja kufanya shughuli zake nchini ikiwemo kutoa misaada.

“Kuanzia sasa serikali inapiga marufuku mashirika na taasisi zinazojihusisha na usambazaji wa vilainishi vinavyochochea mapenzi ya jinsia moja kwa madai ya kuwa wanapunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi,” alisema Ummy.

Alisema kutokana na utafiti uliofanywa na wizara ya afya hivi karibuni unaonyesha kuwa wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja ni asilimia 40 na wanawake ni asilimia 37 hapa nchini.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.