Mkandarasi anyang’anywa kazi ya kusambaza umeme

MZALENDO - - MBELE - NA MWANDISHI WETU, MPANDA

SERIKALI imeamua kukamilisha kazi ya usambazaji umeme wilayani Mlele, iliyokuwa ikifanywa na kampuni ya Lucky Export ya India, ambayo ametelekeza kazi hiyo na kuahidi kumchukulia hatua za kisheria mkandarasi huyo. Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani alitangaza uamuzi huo kwa wananchi wa Kijiji cha Inyonga, Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, juzi, wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme wilayani humo.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri alifuatana na uongozi wa Mkoa wa Katavi na Wilaya ya Inyonga pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Dk. Kalemani alijionea vifaa mbalimbali vya kuunganishia umeme vikiwa vimetelekezwa na kutokuwepo na dalili inayoonyesha kazi kuendelea.

Naibu Waziri alisema kwa kuwa mkandarasi ameshindwa kufanya kazi yake ipasavyo, aliyoianza Novemba 2014 na iliyotarajiwa kukamilika Juni 30, mwaka huu, lazima serikali iingilie kati ili kuhakikisha wananchi wa eneo hilo wanapata huduma ya umeme mapema iwezekanavyo.

“Kuanzia sasa nawaagiza TANESCO kwa kushirikiana na REA, waifanye kazi iliyosalia wao wenyewe, usiku na mchana na ndani ya siku 15 iwe imekamilika ili wananchi mpate umeme kama mlivyotarajia,”aliagiza.

Naibu Waziri alimwagiza Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Katavi, Wambura Nsiku, kuhakikisha mkandarasi huyo halipwi fedha iliyokua imebaki kwani kazi iliyosalia itafanywa na serikali.

Aidha, aliongeza kuwa, serikali itamchukulia mkandarasi huyo hatua nyingine zaidi za kimkataba kwa mujibu wa sheria.

Akizungumzia kuhusu mikakati ya serikali ya kuwapatia wananchi wa Mlele umeme, Dk Kalemani alisema maandalizi ya kuandaa uwanja ambapo jenereta kubwa ya kuzalisha umeme itafungwa, yataanza Agosti Mosi mwaka huu.

Alisema vijiji 95 vya Wilaya ya Mlele ambavyo havikuingia katika mpango wa kupatiwa umeme wa REA awamu ya pili, vitapatiwa nishati hiyo katika mradi wa awamu ya tatu ambao utekelezaji wake umekwishaanza tangu Julai Mosi, mwaka huu.

“Vijiji hivyo vitapata umeme kuanzia mwezi Septemba mwaka huu, lakini tutaendelea kuvisambazia kwa muda wa miaka miwili na nusu hadi mitatu, hivyo ndani ya muda huo, Mlele vitakuwa vimeshapata umeme.”

Vilevile, Naibu Waziri alieleza kuwa, kuanzia Januari mwaka ujao, serikali itaanza kutekeleza mradi wa umeme wa maji kwenye mto Malagarasi ambao unatarajiwa kuzalisha megawati 44.8.

Alisema mradi huo, utawezesha kuondokana na umeme wa jenereta wa kutumia mafuta, badala yake utatumika umeme wa maji ambao ni wa uhakika zaidi.

Aidha, aliwataka wananchi wa Mlele, pindi watakapopata umeme, wautumie vizuri kwa ajili ya shughuli mbalimbali kwa maendeleo yao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.