Kapteni wa JWTZ apanda kortini kwa kutishia kuua

MZALENDO - - MBELE - NA SYLVIA SEBASTIAN

KAPTENI wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Henrick Mahenge (34), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, kujibu shitaka la kujaribu kuua.

Mahenge alifikishwa mahakamani hapo juzi mbele ya Hakimu Mkazi, Mwandani Hassan, kisha kusomewa shitaka hilo na Wakili wa Serikali Grace Mwanga.

Grace alidai mshitakiwa alitenda kosa hilo Julai, 12 mwaka huu maeneo ya Mnazi Mmoja wilaya ya Ilala.

Alidai mshitakiwa alimtishia kumuua kwa kumgonga na gari Konstebo wa Polisi, Cresensia Makanyanga na kumsababishia maumivu mwilini.

Mshitakiwa hakuruhusiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi bado haujakamilika, lakini shauri hilo linadhaminiwa kwa mujibu wa sheria na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Hassan alimtaka mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili kutoka taasisi inayotambulika kisheria watakaotia saini bondi ya sh. milioni mbili kwa kila mdhamini ambapo kesi itatajwa Julai 19, mwaka huu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.