TBS yanasa kiwanda bubu cha mafuta Dar

MZALENDO - - HABARI - NA MUSSA YUSUPH

KIWANDA bubu cha kutengeneza mafuta na vilainishi vya injini za magari na mitambo, kimefungiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) baada ya kubainika kuzalisha bidhaa hizo pasipo kuzingatia sheria.

Kiwanda hicho kilibainika kuwepo kwenye duka la Temeke Ba eries and Lubricants lililopo Temeke Mwisho, Dar es Salaam ambapo TBS ililazimika kuchukua sampuli za bidhaa hizo kwa uchunguzi zaidi.

Ofisa Viwango wa shirika hilo, Safari Fungo, alisema walikibaini kiwanda hicho juzi wakati walipofanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye duka hilo kwa ushirikiano na polisi.

Alisema ukaguzi huo ulilenga kuhakikisha vilainishi pekee vinavyoendelea kuingizwa na kuuzwa kwenye soko la ndani ni vyenye ubora unaokubalika.

“Tulifika katika duka hilo kuhakikisha kuwa ubora wa vilainishi vinavyouzwa vinapaswa kuendana na matakwa ya viwango vya ubora nchini, lakini tulipoingia ndani ya duka hilo tulikuta uzalishaji wa vilainishi unaendelea na kwenye mazingira yasiyofaa, hivyo kulazimika kufunga kiwanda hicho,”alisema.

Fungo alisema mazingira duni ya kiwanda hicho kwenye uzalishaji wa vilainishi na aina ya malighafi wanayotumia kutengenezea ndivyo vilivyowasukuma kuchukua sampuli kwa ajili ya kuipima kwenye maabara ya shirika hilo.

Alisema vilainishi vinavyouzwa katika duka hilo vinazalishwa kiholela kwa kuchanganywa oil chafu, dizeli na vilainishi vingine jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa injini za magari, mitambo.

Hata hivyo, wahusika wa kiwanda hicho walijitetea kuwa wanatumia malighafi salama na kwamba wanazinunua kwa ujazo wa mapipa na kulazimika kufanya uchanganyaji kwa kutumia chupa za maji na ndoo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.