Abambwa na sare za jeshi

MZALENDO - - HABARI - NA LATIFA GANZEL MOROGORO

POLISI mkoani Morogoro inamshikilia Deodatus Simba (26) mkazi wa Dar es Salaam kwa tuhuma za kukutwa na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ulrich Matei, alisema mtu huyo alikamatwa Julai 13, mwaka huu saa 10 jioni maeneo ya Msamvu katika Stendi Kuu ya mabasi mkoani Morogoro.

Alisema mtuhumiwa alikamatwa akiwa amevaa sare hizo wakati akiwa katika harakati za kutafuta usafiri wa kwenda Dodoma.

Matei alisema uchunguzi wa awali uliofanywa na jeshi hilo umebaini kuwa mtu huyo hakua askari wa JWTZ na kwamba atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Awali, mtuhumiwa huyo alipohojiwa na waandishi wa habari alidai nguo hizo ni za kaka yake anayefanya kazi katika kikosi cha Maramba mkoani Tanga.

“Nilikuwa nakwenda Dumila kwa kaka yangu mwingine kumwomba pesa ila sikuwa na nauli ndio maana niliamua kuvaa nguo hizi ili kuweza kupata usafiri wa bure,íí alisema mtu huyo.

Mtuhumiwa huyo alidai yeye ni mfanyabishara wa mitumba jijini Dar es Salaam na kwamba kaka yake ambaye ni mwanajeshi alikuwa amekwenda Dar es Salaam na kuziacha sare hizo nyumbani, hivyo mtuhumiwa huyo aliamua kuzivaa.

Hata hivyo, alikiri anatambua kuvaa sare hizo wakati yeye si mwanajeshi ni kosa , lakini hakujua kama angepatikana katika mazingira hayo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.