Kanisa kufanya maombi siku 100 kuliombea taifa

MZALENDO - - HABARI/ TANGAZO - NA SYLVIA SEBASTIAN

ASKOFU wa Kanisa la Good News for All Ministry, Charles Gadi, amezindua maombi ya siku 100 yatakayofanyika nchi nzima kila Jumanne.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Askofu Gadi alisema mkutano huo utazinduliwa katika Viwanja vya Biafra na mambo 16 yataombewa kwa ajili ya kufanikisha taifa katika utendaji wa Rais Dk. John Magufuli.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni kuhamasisha wananchi wote kupitia njia ya maombi, kuwa na utayari wa kulipa kodi na ushuru ili kukuza uchumi na maendeleo ya nchi jambo ambalo ni uzalendo kwa nchi.

Pia, kuhamasisha wananchi kujiunga na mifuko ya jamii na taasisi ndogo za fedha kama vile vikoba, SACCOS na benki ili kuweza kuwawekea akiba na uwezekano wa kukopesheka kwa ajili ya maendeleo ya mtu mmoja na jamii kwa ujumla.

“Kuombea na kuhamasisha wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya taifa kama vile barabara, shule, hospitali, madaraja, reli, viwanja vya ndege, majengo ya serikali ili viweze kudumu kwa muda mrefu.

“Kuhamasisha kupitia mikutano ya maombi juu ya matumizi bora na endelevu ya ardhi yetu ili iweze kusaidia vizazi vijavyo kwa sababu watu wanaongezeka ila ardhi ni ileile, kuhamasisha utalii wa ndani na uhifadhi wa mbuga za wanyama sambamba na kumuomba Mungu aingilie kati ili kukomesha ujangili na uuaji wa wanyama,” alisema.

Alisema maombi hayo tena yatalenga kuwahamasisha wananchi kuchunguza afya zao mara kwa mara na kuhamasisha wananchi mijini na vijijini kutumia njia za kisasa za mawasiliano ili kupata taarifa sahihi zinazohusu kazi, kilimo na afya ili kuongeza ufanisi.

Pia, kuwahamasisha wananchi kuwa na tabia ya kujiwekea kumbukumbu za hesabu za kila siku ikiwa ni pamoja na kuomba na kutunza risiti za manunuzi yao, kujiepusha na tabia zenye kuleta mmomonyoko wa maadili kwa watu wazima na watoto na kuimarisha ubora wa vyakula na vinywaji.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.