IGP Mangu avisha nishani

MZALENDO - - HABARI - NA SYLVIA SEBASTIAN

MKUU wa Jeshi la Polisi Nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu, amewavisha nishani ya shirikisho la wakuu wa polisi wa nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO) na wakuu wawili wa jeshi la polisi wastaafu.

Pia amewavisha nishani maofisa wanne wa Jeshi la Polisi Tanzania.

IGP Mangu amewavisha nishani hizo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Shirikisho hilo Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Msumbiji.

Taarifu iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Advera Bulimba, iliwataja waliovishwa nishani kuwa ni Inspekta Jenerali wa Polisi mstaafu, Omari Mahita ambaye alikuwa IGP wa kwanza nchini kuwa mwenyekiti wa shirikisho hilo.

Mwingine ni IGP mstaafu Said Mwema ambaye akiwa mwenyekiti wa shirikisho alifanikiwa kuunganisha operesheni za pamoja kati ya EAPCCO na SARPCCO ambazo zinaendelea kutekelezwa hadi sasa.

Pia, maofisa wengine waliovishwa nishani ya kulitumikia vizuri shirikisho hilo ni DCP Nassoro Laisseri, ambaye alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Interpol Tawi la Tanzania.

Mwingine ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Afwilile Mponi, ambaye alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Usafirishaji Haramu wa Binadamu.

IGP Mangu, aliwavisha nishani ya ushiriki vizuri katika operesheni za kikanda kwa nchi za Kusini mwa Afrika, maofisa wa polisi wawili ambao ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mstaafu, Godfrey Nzowa na Mrakibu wa Polisi Heri Lugaye.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.