Atozwa sh. milioni moja kwa kumiliki dhahabu kinyemela

MZALENDO - - HABARI - NA FURAHA OMARY

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu mfanyabiashara Christian Richard, kulipa faini ya sh.milioni moja au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumiliki gramu 901 za dhahabu bila kibali.

Richard alipewa adhabu hiyo na Hakimu Mkazi Mkuu, Emmilius Mchauru, baada ya kukubali kosa hilo alilosomewa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga.

Akimsomea shitaka, Katuga alidai mshitakiwa alitenda kosa hilo, Desemba 31, mwaka jana, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, ulioko wilayani Ilala, mkoa Dar es Salaam.

Katuga alidai, mshitakiwa huyo akiwa uwanjani hapo alikutwa na gramu 901 za madini aina ya dhahabu bila ya kuwa na kibali kutoka mamlaka husika.

Mshitakiwa huyo baada ya kusomewa shitaka hilo alikiri ambapo Hakimu alimpa adhabu hiyo ya kulipa faini ya sh. milioni moja au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.

Mfanyabiashara huyo aliweza kunusurika kutumikia adhabu hiyo ya kifungo baada ya kulipa faini na kuachiwa huru.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.