Waliolipwa fidia sasa watakiwa kuondoka

MZALENDO - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Joseph Nyamhanga, amewataka wakazi wa Arusha ambao wameshalipwa fidia kupisha ujenzi wa barabara ya Arusha Bypass kuboa nyumba zao haraka ili ujenzi wa barabara hiyo uanze mara moja.

Akizungumza baada ya kukagua barabara hiyo ya Arusha Bypass inayoanzia TPRI - Ngaramtoni - Oljoro hadi USA River yenye urefu wa kilomita 42.4, Mhandisi Nyamhanga, aliwataka wakazi wanaopitiwa na ujenzi wa barabara hiyo kupisha eneo la ujenzi ili kumwezesha mkandarasi kuanza kazi.

“Ni vema wananchi ambao mmeshalipwa fidia mkabomoa nyumba zenu wenyewe ili kupisha eneo la ujenzi kwani tayari kiasi cha sh. bilioni 21 kimetolewa na serikali kwa ajili ya fidia ili kuharakisha ujenzi wa barabara hii”, alisema.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo alimtaka mkandarasi anayejenga barabara ya Sakina - Tengeru yenye kilomita 14.2 kuongeza kasi ya ujenzi ili kumaliza ujenzi huo ndani ya mkataba.

“Hakikisheni ujenzi wa barabara ya Arusha Bypass unaenda sambamba na kukamilika kwa barabara ya Sakina - Tengeru ili kuondoa msongamano katika barabara kuu ya Arusha - Moshi, alisisitiza.

Barabara ya Arusha Bypass yenye kilomita 42.4 na Sakina Tengeru kilomita 14.2 ni sehemu ya barabara kuu ya Arusha Moshi - Holili - Taveta hadi Voi yenye nia ya kupunguza msongamano katika ukanda wa kaskazini inajengwa na Kampuni ya Hanil na Jangsu kutoka Korea Kusini na China.

Barabara hiyo ya Arusha Bypass na Sakina - Tengeru zitakapokamilika zinatarajiwa kuwa na madaraja makubwa saba na Makalvati 26 ambapo zaidi ya sh. bilioni 164.4 zimetolewa na Benki ya Maendeleo Afrika na Serikali ya Tanzania kugharamia ujenzi huo.

Kukamilika kwa barabara hiyo licha ya kupunguza msongamano katika mji wa Arusha na Moshi pia kutakuza sekta ya utalii katika ukanda wa kaskazini mwa Tanzania.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.