Jengeni barabara za lami-Mongella

MZALENDO - - HABARI -

MIUNDOMBINU thabiti ya kiuchumi ikiwemo barabara na vivuko, ndiyo itakayo liwezesha taifa kufikia malengo ya kujenga Tanzania yenye viwanda, imeelezwa.

Ili kutimiza azma hiyo mkoani Mwanza, halmashauri za wilaya, Manspaa na Jiji la Mwanza zimetakiwa kutongíangíania kujenga barabara za vumbi, bali zijikite kwenye ujenzi wa barabara za lami.

Ushauri huo umetolewa juzi na Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella, wakati akifungua na kufunga kikao cha Bodi ya Barabara ya mkoa huo, kilichofanyika jijini hapa.

Mongella alisema hataki hadithi za mara kwa mara zinazotolewa na halmashsuri hizo, kwa kuwa wana-Mwanza wanataka kuona utekelezaji wa ujenzi wa barabara hivyo kauli za blabla hazina nafasi katika serikali ya awamu ya tano.

“Msibaki kwenye barabara za lami zilizo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), wananchi wa Mwanza wanataka barabara na vivuko, kila Halmashauri ianze kutengeneza kilomita mbili hadi tatu za lami kila mwaka ili tuepukane na barabara za vumbi.

“Fedha za Mfuko wa Barabara za mwaka huu zisiishie kwenye barabara za vumbi tu (moramu), wakurugenzi, wabunge na wenyeviti wa Halmashauri zote nendeni mkaanze ujenzi wa barabara za lami,”aliagiza RC Mongella.

Mongella alisisitiza kuwa miundombinu thabiti ya kiuchumi ikiwemo barabara na vivuko, ndiyo itakayo liwezesha taifa kufikia malengo ya kujenga Tanzania na Mwanza yenye viwanda hivyo halmashauri zote zizingatie hilo.

Awali katika kikao hicho wenyeviti na wakurugenzi wa wilaya za Magu, Misungwi, Buchosa, Sengerema, Ukerewe na Kwimba ‘walililia’ kupandishwa hadhi kwa baadhi ya barabara za halmashauri zao na kuwa chini ya Tanroads mkoa wa Mwanza.

Walisema baada ya kuanzishwa mikoa mipya ya Simiyu na Geita, baadhi ya barabara zilizokuwa Mwanza zimechukuliwa na Tanroads kwenye mikoa hiyo, hivyo Mwanza kupunguziwa mzigo na kwamba ni muhimu sasa kwa mkoa huo kuzipandisha hadhi baadhi ya barabara ili fedha zinazotolewa na serikali mkoani humo ziendelee kuboresha barabara zingine.

Akijibu maombi hayo, Kaimu Mhandisi wa Tanroads mkoani Mwanza, Felix Ngaile, alisema viongozi hao wanapaswa kujitahidi kuomba fedha kutoka Mfuko wa Barabara kwa kuwa wanao wataalamu wanaoweza kufanya kazi nzuri.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.