JPM: Wananchi wasitozwe kodi ambazo ni kero

Wabunge, madiwani waagizwa kubuni miradi ya maendeleo

MZALENDO - - MBELE - NA ABDALLAH AMIRI, IGUNGA

RAIS Dk. John Magufuli, amewaagiza viongozi katika ngazi mbalimbali kuhakikisha wananchi hawatozwi kodi ambazo ni kero.

Amesema hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba kufutwa kwa kodi hizo ni ahadi iliyotolewa wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara kwenye mnada wa mjini Igunga, Rais Dk. Magufuli alisema kumekuwa na tabia ya wananchi kutozwa ushuru ambao ni kero kwao na kuwataka viongozi wasimamie ili wananchi wasiteseke.

Alitoa mfano wa mkulima anayepeleka magunia machache ya mpunga nyumbani kwake na kutozwa ushuru au mwananchi kuwa na mbuzi kwa shughuli binafsi na kutozwa ushuru kuwa ni kero kwa wananchi.

Pia, alirudia wito wake kwa wananchi kutii sheria pasipo shuruti huku akimwaagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na viongozi ndani ya Jeshi la Polisi kuwafuatilia wachache wasio na maadili na kuwashughulikia.

Akizungumzia miradi ya maendeleo. Rais Dk. Magufuli aliwataka viongozi katika ngazi mbalimbali nchini kubuni miradi ya maendeleo kwa lengo la kutatua kero za wananchi na si kusubiri miradi ya kitaifa.

Rais Dk. Magufuli alisema wabunge, madiwani, watendaji na wenyeviti wote wa serikali za vijiji wanatakiwa kushikamana na kubuni miradi ya maendeleo katika vijiji na kata zao ili kuharakisha maendeleo ya wananchi katika maeneo yao.

Alisema wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana alitoa ahadi mbalimbali kwa wananchi na utekelezaji wa ahadi hizo tayari umeanza kwa kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi la saba na kidato cha kwanza hadi cha nne ikiwemo kumaliza changamoto ya madawati, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ikiwemo kufuta safari za nje ya nchi mpaka kwa kibali maalumu.

Alisema serikali yake imeweka mkakati mkubwa wa kukusanya mapato kutoka vyanzo mbalimbali jitihada ambazo zimeleta mafanikio makubwa sambamba na kuanzisha mahakama maalumu ya kushughulikia mafisadi ili kuwachukulia hatua wote wanaojihusisha na vitendo vya wizi wa mali ya umma na uhujumu uchumi.

Licha ya jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na serikali yake katika kutatua kero za wananchi, Rais Magufuli alisema bado zipo changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao na kubainisha kuwa jitihada zinaendelea kufanywa kukabiliana nazo.

Ili kufanikisha jitihada za serikali katika kutatua kero za wananchi, aliwataka wenyeviti na watendaji wote wa serikali za vijiji kwa kushirikiana na madiwani na wabunge kubuni miradi katika maeneo yao itakayowezesha kutatua kero za wananchi.

Aliwataka kupanga mikakati mbalimbali itakayosaidia kumaliza changamoto zilizoko katika halmashauri zao wakati serikali ikiendelea kuweka utaratibu mzuri wa kutatua changamoto kubwa.

Wakati huo huo, Rais Dk. Magufuli leo anatarajiwa kuunguruma katika Uwanja wa Kalangalala mjini Geita ambapo atahutubia maelfu ya wananchi wa mji huo na vitongoji vyake.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstafu, Ezekiel Kyunga, Rais Dk. Magufuli anatarajiwa kuwasili hapa leo mchana akitokea mkoani Shinyanga.

Alisema baada ya kuhutubia wananchi wa Geita, kesho asubuhi atawahutubia wananchi wa mji mdogo wa Katoro uliopo mpakani mwa wilaya za Geita na Chato, wakati akiwa njiani kwenda nyumbani kwake katika Kijiji cha Lubambagwe wilayani Chato.

RAIS Dk. John Magufuli akiwa na wabunge wa Mkoa wa Singida akiwahutubia wakazi wa Misigiri mkoani Singida, jana wakati akielekea Mkoani Tabora katika ziara ya kikazi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.