Dk. Mpango akutana na Makamu wa Rais AfDB

MZALENDO - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dk. Frannie Leautier.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Mpango aliishukuru benki hiyo kuwa mojawapo ya mashirika ya kimataifa yanayoisaidia Tanzania katika sekta za maendeleo.

Benki hiyo imewekeza nchini kiasi cha dola Bilioni 2 (zaidi ya sh. trilioni 4.4) kama ruzuku na mikopo yenye riba nafuu ili kuendeleza sekta mbalimbali ikiwemo barabara, elimu, kilimo, nishati ya umeme, na viwanda.

Dk. Mpango, alisema amefurahishwa na dira ya AfDB ambayo inafanana na vipaumbele vya serikali, kupitia Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano ambao umelenga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025.

Dira ya benki hiyo imejikita katika malengo matano ambayo ni kuwekeza katika nishati ya umeme, uzalishaji wa chakula, kuendeleza viwanda, kuiunganisha Afrika kwa mtandao wa barabara na kuboresha maisha ya watu.

Dk. Mpango alisema uwekezaji katika sekta hizo utasaidia mpango mkubwa wa uboreshaji wa miundombinu kama vile kujenga viwanda kwa kuhusisha sekta ya umma na binafsiPPP, umeme wa kutosha kuendesha viwanda, barabara ambazo zitaunganisha nchi zote za Afrika.

“AfDB wametusaidia sana katika ujenzi wa barabara nyingi nchini Tanzania ikiwemo barabara ya kutoka Tanga kwenda Horohoro, ambayo imerahisisha usafiri wa kwenda nchini Kenya. Barabara nyingine zitajengwa kutoka mpakani Kagera kupitia Kigoma kwenda Katavi, Dodoma hadi Iringa. Hili ni jambo kubwa” Alisema Dk. Mpango

Dk. Mpango alimweleza Makamu huyo wa Rais wa AfDB, juu ya mpango wa serikali wa kuimarisha sekta ya usafirishaji ikiwemo kujenga Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge) ambapo sh. trilioni 16 zinahitajika kukamilisha mradi huo.

Alisema tayari serikali imetenga kiasi cha sh. trilioni moja katika bajeti yake ya mwaka huu 2016/2017 kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi huo mkubwa unaohusisha njia ya reli yenye urefu wa kilometa 2,190.

Alitaja sekta nyingine ya kipaumbele kuwa ni kilimo kwa ajili ya kuzalisha chakula kwa wingi lengo likiwa kutosheleza matumizi ya ndani na ziada yake kuuzwa nje ya nchi huku ikitiliwa mkazo uzalishaji wa malighafi zitakazotumika katika viwanda.

Kwa upande wake, Dk. Leautier ambaye aliambatana na mwakilishi mkazi wa benki hiyo, Tonia Kandiero, alisema AfDB imesaidia na itaendelea kusaidia miradi ya maendeleo hapa nchini ikiwemo ya barabara, elimu, kilimo, afya, sekta ya umeme ili Tanzania iwe na umeme wa kutosha kuendesha viwanda.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Spika wa Bunge, Job Ndugai, nyumbani kwa Spika, Dar es salaam, juzi baada ya kurejea nchini hivi karibuni akitokea India kwa matibabu. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama. (Picha na Ofisi ya Bunge).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.