Walioifilisi Nyanza kuchukuliwa hatua

MZALENDO - - HABARI - NA PETER KATULANDA, MWANZA

VIGOGO wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Mwanza, Nyanza Cooperative Union Ltd (NCU 1984 Ltd), waliouza mali za chama hicho kwa bei chee na kutafuna mamilioni ya fedha zake, wanachunguzwa upya ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Viongozi hao ni wale wa zamani, waliouza majengo, viwanja na viwanda chini ya thamani halisi ya mali hizo na kunufaisha matumbo yao, pamoja na wapya waliosimamishwa Julai 15 mwaka huu kufuatia agizo la Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Dk. Charle Tizeba kwa Mrajis wa Vyama Vya Ushirika nchini.

Akijitambulisha kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mwanza (RCC) kilichofanyika juzi jijini Mwanza, Kaimu Mteandaji Mkuu mpya, Juma Mokili, alisema serikali imetoa maelekezo ya kushughulikia suala hilo kwa umakini.

Mokili ambaye ni Mrajisi Msaidizi Kitengo cha Ushirika na Mkaguzi Mkuu wa Vyama vya Ushirika, anakaimu nafasi hiyo baada ya Bodi na Menejmenti ya NCU kuvunjwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk Audax Rutabanzibwa, baada agizo hilo.

“Nimeelekezwa kuunda bodi ya mpito baada ya iliyokuwepo kuvunjwa kwa maagizo ya Waziri wa Kilimo, Ushirika na Maendeleo ya Mifugo, Dk. Tizeba hivi karibuni na tayari hatua zimechukuliwa.”

“Nyanza haijafa bali imesinzia, tunataka kuiamsha irudi kwenye mfumo wa zamani wa Victoria Nyanza Federation Union, maana wakulima wa pamba wananyanyasika na bei baada ya mali zake kufujwa na viongozi waliokuwepo ,î alisema Mokili.

Alifafanua kuwa, vigogo waliokuwa madarakani kwa nyakati tofauti wameanza kuchunguzwa kuona thamani ya mauzo ya mali za Nyanza ina uhalisia na iwapo ziliuzwa kwa kufuata taratibu.

Kaimu Mtendaji Mkuu huyo alisema: ìNimeteuliwa kufanya yafuatayo, moja ni kushirikiana na wachunguzi, Kamati ya Ulinzi na Usalama, kupata bodi mpya, Mtendaji Mkuu na kuunda mpango wa kuiamsha Nyanza kutoka usingizini kama yalivyo maelekezo ya serikali,î

Mokili alikiri kuwa kazi hiyo ni ngumu na peke yake hataiweza, hivyo kuomba ushirikino kwa wadau, serikali na taasisi zake kwani historia inaonyesha kuwepo vitisho na ugumu katika kuwabaini wahusika wa hujuma na ubadhirifu wa ndani ya Nyanza.

Habari zilizopatikana jijini hapa zilisema hatua hiyo inatokana na Rais Dk. John Magufuli, ambaye amewahi kufanya kazi Nyanza, kuwa hataki ushirika huo upotee wakati wakulima wanaendelee kulanguliwa.

Mokili alisema ameagiza uchunguzi ufanyike na taarifa itolewe ili serikali ichukue hatua kwa wahusika na kurejesha mali zilizouzwa kinyemela na kwa bei ya kutupa.

Akithibitisha maagizo hayo ya serikali wakati akifunga kikao hichocha RCC, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema yeyote aliyehusika kufanya ubadhirifu wa mali za Nyanza, hatapona.

Mongella alimwagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama na kikosi kazi kufanya uchunguzi wa kina kubaini vigogo waliohusika kuuza mali za NCU kwa bei chee kinyume cha utaratibu na bila kuzingatia thamani halisi ya mali hizo.

ìYawezekana wapo walioapa kufia Nyanza, mimi na wenzangu serikalini tumejipanga kutekeleza maelekezo ili mali za wakulima zirudi na kuwanufaisha wenyewe wana Mwanza,î alisema Mongella na kumhakikishia ulinzi Kaimu Mtendaji Mkuu mpya wa Nyanza.

Mongella alisema alishangaa wakati akipitia nyaraka za Nyanza na kuona kiwanda cha New Era kilichopo eneo la Voil kuuzwa kwa sh. milioni 30 zilizowekwa benki wakati thamani yake ikiwa zaidi ya sh.bilioni moja, huku mnunuzi akikikodisha kwa sh.milioni 10 kila mwezi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.