Mbunge Ester agawa madawati 90 Bunda

MZALENDO - - HABARI - NA AHMED MAKONGO, BUNDA

MBUNGE wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, ametoa msaada wa madawati 90 kwa Shule za Msingi, Nyatwali, Rigamba ëAí na Nyerere mkoani Mara. Ester alitoa msaada huo katika Halmashauri ya Mji wa Bunda ambako shule hizo zipo.

Akitoa msaada huo, juzi, Ester alisema si vyema watoto kusoma wakiwa wamekaa chini na kwamba madawati hayo yametokana na mfuko wa jimbo hilo.

Mbunge huyo alisema wakati wa ziara yake aligundua kuna changamoto nyingi katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na upungufu wa madawati katika shule za msingi na kwamba hicho ndicho kilichomsukuma kutumia mfuko huo wa jimbo kuchangia madawati hayo.

Ester alisema atachangia madawati mengine 500 kama mbunge wakati zamu yake itakapofika na anachokisubiri ni kuandikiwa barua na uongozi wa bunge ili kutekeleza agizo hilo la Rais Dk. John Magufuli.

“Ikifika zamu yangu nitachangia hapa nilipo ninasubiri barua tu ili niweze kuchangia madawati hayoÖunajua mambo ya maendeleo hayana itikadi za vyama wala za kisiasa,” alisema.

Kwa upande wao, walimu katika shule hizo, wakiongozwa na Mwalimu wa Shule ya Msingi Nyatwali, Thomas Magesa, alisema wanakabiliwa na upungufu wa madawati na kwamba wanafunzi 153 wanasoma wakiwa wamekaa chini.

Walisema upungufu huo wa madawati katika shule hizo imekuwa ikisababisha baadhi ya wanafunzi kuwa watoro na kuwepo kwa uhusiano usiofaa kati ya walimu na jamii kwa kufikiri kwamba upungufu wa madawati unasababishwa na walimu wa shule husika.

Akipokea madawati hayo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Janeth Mayanja, alimshukuru mbunge huyo huku akiwaomba wadau wengine kuchangia madawati.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.