CCM wilaya ya Temeke yatambia Kigamboni

MZALENDO - - HABARI - NA CHRISTOPHER LISSA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Temeke, imewatoa wasiwasi wananchi wa wilaya mpya ya Kigamboni kwamba Chama kimejipanga kikamilifu kuichukua wilaya hiyo katika ngazi zote, ikiwemo nafasi ya mstahiki meya.

Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Yahaya Shaban, alisema juzi kuwa wana uhakika meya atakayeiongoza Kigamboni atatokea CCM na aliwataka wananchi wawe na amani.

Alisema wamejihakikishia ushindi huo kutokana na takwimu ya kufanya vizuri, Kigamboni na kwamba uchaguzi wa mameya wilayani humo ukiitishwa wakati wowote wapinzani wajiandae kwa kipigo kitakatifu.

“Tuna uhakika na tumejipanga kuusambaratisha upinzani kabisa Kigamboni katika uchaguzi wa umeya. Wananchi wawe na amani tu. Si kwa sababu ya nini tutafanya, ila kwa sababu ya takwimu.

“Katika uchaguzi mkuu uliopita, kwenye wilaya ya Kigamboni CCM ilichukua kata nyingi, ambazo ni Kibada, Kigamboni, Kisarawe two, Somangila, Kimbiji na Pemba Mnazi ambapo wapinzani walichukua kata tatu tu ambazo ni Mji Mwema, Tungi na Vijibweni,”alisema.

Alisema idadi hiyo ya madiwani, ukijumlisha na mbunge na viti maalumu, wajumbe wanafikia 10, hali inayoonyesha ushindi dhahiri kwa CCM.

“Hii inaonyesha ni jinsi gani CCM imefanya vizuri kupitia Wilaya ya Temeke, lakini kazi hii haikufanywa na viongozi tu wa Chama, bali wanaCCM na wananchi,”alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.