Mangula afichua siri ya kuitwa ‘Mzee wa Mafaili’

MZALENDO - - MBELE - NA WILLIAM SHECHAMBO

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip Mangula, amemtembelea aliyekuwa Katibu wa kwanza wa Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere, Paul Sozigwa na kufichua siri ya chanzo cha kuitwa jina la ‘Mzee wa Mafaili’.

Alisema jina hilo linalojulikana sana ndani ya Chama, lilitokana na ushirikiano aliokuwa nao kati yake, mzee Sozigwa na wajumbe wengine wa sekretarieti ya CCM,

ambapo kila mgombea alikuwa anafunguliwa faili maalumu la mazuri na mabaya yake.

Mangula alisema kwa kipindi cha miaka 10, akiwa Katibu Mkuu wa CCM mpaka 2006, alifanya kazi kwa mafanikio na sekretarieti iliyokuwa madarakani ambapo Kamati ya Maadili alimkabidhi Sozigwa aiongoze.

Alisema mzee Sozigwa na wengine akiwemo Kanali Mhando na Kapteni Tualani walisimamia misingi na kanuni zilizokuwepo, hivyo kufanya mchakato wa kumpata mgombea urais kwa uchaguzi mkuu kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Makamu Mwenyekiti wa CCM aliwasili nyumbani kwa mzee Sozigwa majira ya saa nane mchana ambapo alipokewa kwa nyimbo za dini alizokuwa akiimba Sozigwa kwa ushirikiano na mkewe na watoto wawili waliokuwepo kwa muda huo.

Sozigwa ambaye ni kada wa miaka mingi wa CCM, alionekana kuwa na furaha iliyopitiliza baada ya kumuona Mangula ambapo mazungumzo yao yalitawaliwa na vicheko wakati wote.

Mara baada ya mazungumzo yao yaliyochukua takriban dakika 45, Mangula alisema amefurahi kumuona Sozigwa akiwa mwenye afya njema baada ya kupoteana naye kwa miaka 10.

“Nimefurahi, tulifanya kazi kubwa, ilikuwa kamati makini ambapo mtu alikuwa akitangaza kugombea nafasi chamani, nilikuwa namfungulia faili maalumu lenye kila kitu, hivyo akipita ilikuwa ni kihalali,” alisema Mangula.

Kwa upande wake Mzee Sozigwa alisema amepata faraja kumuona Makamu Mwenyekiti huyo, ambapo wakati wote alitamani kuonana naye baada ya kupotezana kwa kipindi cha miaka 10.

Alisema kiafya anaendelea vizuri ambapo kwa sasa muda mwingi anatumia kuimba nyimbo za dini kama ilivyo desturi yake tangu ujana, kiasi cha kumpa mwanae wa pili jina la Imbeni.

Miaka ya sabini, Sozigwa akiwa Mkurugenzi wa Redio Tanzania (RTD), alianzisha kipindi cha redio kilichojulikana kwa jina la ‘mikingamo’ ambapo pamoja na mambo mengine kilitoa mchango mkubwa kwenye kuhabarisha umma wakati wa Vita ya Kagera.

ASKARI polisi vikosi vya Kikosi Maalum (CRT) na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wa mikoa mbalimbali wakifanya mazoezi ya utayari kupambana na matukio ya uhalifu na wahalifu. (Picha zote na Makao Makuu ya Jeshi la Polisi).

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula (kushoto), akiagana na mwanasiasa mkongwe nchini, Paul Zosigwa, baada ya kumjulia hali nyumbani kwake, Magomeni Mapipa, Dar es Salaam, jana. Katikati ni mke wa Sozigwa, Monica. (Na Mpigpicha Wetu).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.