Simbachawene ataka udhibiti wa elimu

MZALENDO - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene amewataka watendaji wanaosimamia uendeshaji wa elimu katika ngazi ya mkoa, halmashauri na shule kuzingatia kwa ukamilifu ushauri unaotolewa na Wadhibiti Ubora wa Elimu.

Akifungua kikao cha siku mbili kati ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa( OR-TAMISEMI) na maofisa elimu wa mikoa, wakuu wa shule kongwe na wakuu wa zilizoungua moto kilichofanyika mjini Dodoma.

Simbachawene alisema kushindwa kufanyia kazi kasoro zinazojitokeza au kutambuliwa na wadhibiti ubora ni sawa na kuhujumu jitihada za serikali za kuwaandalia maisha bora vijana wake.

“Nitumie wasaa huu, kuwaagiza watendaji wote mnaohusika katika eneo hilo kushughulikia kikamilifu kasoro zote zinazotambuliwa hususani zile ambazo ziko ndani ya mamlaka za uwezo wenu na kama ziko juu ya uwezo wenu, basi ziwasilisheni kwa wakati kwa mamlaka husika,”alisema Simbachawene.

Alisema serikali ya awamu ya tano imeifanya elimu kuwa ni moja ya vipaumbele vyake na kuwekeza mabilioni ya fedha katika kuendesha na kutekeleza miradi ya elimu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ambapo miongoni mwa mambo ambayo serikali imeyafanya katika kuboresha elimu nchini ni kuwaendeleza walimu.

Waziri huyo alisema serikali inawaendeleza walimu kupitia mipango mbalimbali, kutoa fedha za ruzuku, kutoa fidia ya ada, chakula na maabara kila mwezi, kuwanunulia pikipiki waratibu elimu wa kata wote, kutengeneza madawati kwa shule za msingi na sekondari, kusambaza vitabu kwa darasa la kwanza na kusambaza vitabu vya sayansi na hisabati kwa shule za sekondari.

Mambo mengine yaliyofanywa na serikali katika kuboresha elimu ni ujenzi wa maabara, ukarabati wa shule kongwe, ukarabati wa shule za ufundi, utoaji wa mafunzo ya uongozi kwa walimu wakuu, wakuu wa shule na waratibu elimu kata na utoaji wa posho ya nadaraka kwa walimu wakuu wa shule na waratibu elimu kata.

Hivyo, alisema kutokana na mambo hayo hakuna sababu za msingi za shule kutofanya vizuri hasa kwa shule kongwe zinaendelea kushuka na baadhi ya shule hizo kuwa za mwisho katika mitihani ya kidato cha sita.

Akizungumzia matukio ya moto, alisema kuungua kwa shule kutokana na ajali za moto ambazo zimekuwa zikitokea hivi karibuni zimekuwa zikiisononesha serikali , wanafunzi, wazazi na watanzania wote kwa ujumla kwa kuwa maeneo yaliyopatwa na majanga ya moto yameathirika kwa kiasi kikubwa.

“Taarifa za uchunguzi za awali ambazo tumekuwa tukizipokea zimeonyesha kuwa chanzo cha ajali nyingi za moto ni hitilafu ya umeme... pamoja na taarifa hizo, tumeendelea kupata mashaka zaidi pale ambapo shule nyingine zilizopatwa na janga la kuungua moto hazina hata miundombinu ya umeme,’’alisema Simbachawene.

Awali, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Bernard Makali, alisema kuwepo kwa udhaifu katika usimamizi wa elimu katika ngazi ya shule ambao umesababisha ufundishaji katika shule kongwe kuwa wa kusuasua na kusababisha shule hizo kushuka kitaaluma na kushika nafasi za mwisho kwenye mitihani ya kitaifa.

Pia, aliwataka washiriki kutumia kikao hicho kupata mbinu sahihi ili kuweza kuinua kiwango cha ufaulu katika shule za serikali na za binafsi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.