Watumishi hewa tatizo

Waongezeka hadi 16,127, watia hasara ya sh. bilioni 16 Wafanyakazi842mikononimwa TAKUKURU, mahakama

MZALENDO - - MBELE - NA EMMANUEL MOHAMED

IDADI ya watumishi hewa imeendelea kuongezeka hadi kufikia 16,127 huku ikiisababisha serikali hasara ya sh. bilioni 16 katika kipindi cha Juni, mwaka huu.

Aidha,sakata hilo limesababisha maofisa utumishi watatu kutumbuliwa kwa kuhusika na uingizwaji wa watumishi hewa kwenye mfumo wa malipo ya mishahara (payroll).

Mbali na hilo, tayari mashauri 236 yamefikishwa mahakamani huku Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ikiendelea kufanya uchunguzi wa kesi 606 za utumishi hewa.

Wakati hayo yakijitokeza, hatma ya taasisi 145 ambazo zimekiuka agizo la Rais Dk. John Magufuli la kuwasilisha taarifa za watumishi hewa ipo mikono mwake ambapo hatua za kisheria na kinidhamu zinatarajiwa kuchukuliwa ifikapo Agosti 26, mwaka huu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejementi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, aliyasema hayo jana mjini Dar es Salaam.

Alisema taasisi hizo zimegawanyika katika makundi kama vile mabaraza mbalimbali 11, bodi mbalimbali 10, vyuo vikuu 25 na hospitali 3.

Angellah aliendelea kuzitaja kuwa kuna Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa 12, mamlaka mbalimbali 6, mamlaka za serikali za mitaa 38, tume 10 na taasisi za umma na wakala 30.

“Miongoni mwa taasisi hizi ni Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE) ,Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE) na Hospitali ya CCBRT, Hospitali ya Rufani ya Bugando na KCMC,”alisema Angellah.

Waziri huyo alizitaja nyingine kuwa ni ofisi za Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Saalam, Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSIR) Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Halmashauri za Jiji la Mwanza na Taasisi ya Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Kituo cha Uwekwezaji Tanzania (TIC).

“Ziko nyingi ila zingine baadhi ni Shirika la Viwango Tanzania(TBS) Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO), Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA)”alizitaja.

Angellah alisema ofisi yake ya menejementi ya utumishi imeongeza muda wa kuwasilisha ambapo Agosti 26, mwaka huu ni siku ya mwisho kwa taasisi hizo kuwasilisha taarifa za watumishi hewa.

Awali, alisema agizo la Rais Dk. Magufuli lilitaka Juni mwaka huu, iwe mwisho wa kuwasilisha taarifa hizo za watumishi hewa, hivyo ni fursa kwa taasisi hizo kuwasilisha kwa kuambatanisha mambo kama vile jina la taasisi husika, fungu, cheki namba ya mtumishi, jina la mtumishi, cheo cha mtumishi, jina la tawi la benki ambalo mshahara wa mtumishi umekuwa ukipitishwa/kulipwa.

“Vilevile bila kusahau akaunti namba ya benki ya mtumishi, tarehe ambayo mtumishi aliondolewa kwenye mfumo wa taarifa ya kiutumishi na mshahara, kiasi cha fedha zilizolipwa kwa mtumishi husika tangu alipotakiwa kuondolewa hadi tarehe aliyoondolewa kwenye mfumo na sababu ya kuondolewa kwa mtumishin kama utoro, kufarik dunia,kuacha kazi, kustaafu na hatua zilizochukuliwa na mwajiri dhidi ya watumishi hewa waliobainika kama kutakiwa kurejesha fedha, maofisa wengine wa taasisi waliosababisha uwepo wa watumishi hewa kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria,”alisema Waziri Angellah.

Aliongeza kuwa waajiri 264 kati ya waajiri wote 409 wamewasilisha taarifa zao kuhusu uwepo wa watumishi hewa na kuwa kati ya waajiri 264 waliowasilisha taarifa zao waajiri 63 wamethibitisha kuwepo kwa watumishi hewa katika taasisi zao na waajiri 201 ndio wana watumishi hewa.

Aidha, alisema kuanzia Agosti 15, mwaka huu ofisi yake inaendelea na uhakiki wa kushtukiza katika taasisi 70 za serikali zikiwemo wizara, idara za serikali zinazojitegemea, sekretarieti za mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na taasisi za umma kwa lengo la kujiridhisha na taarifa za watumishi hewa zilizowasilishwa na waajiri kuwa ni sahihi.

Waziri Angellah alisitiza kuwa taasisi hizo zinapaswa kutambua kuwa Agosti 26, mwaka huu itakuwa mwisho na kwamba ikizidi siku hiyo ofisi yake itawasilisha taarifa ya watumishi hewa kwa Rais ikiwa na orodha na majina ya taasisi ambazo zimewasilisha taarifa ya watumishi hewa na zile ambazo hazijawasilisha.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.