TFS yatoa miche ya miti kumuunga mkono Makonda

MZALENDO - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), imechangia miche 3,000 ya miti katika kampeni ya upandaji miti jijini Dar es Salaam iliyozinduliwa jana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na vyombo vya habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mtendaji Mkuu wa (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, alisema hatua hiyo ni kuunga mkono kampeni ya Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda “Mti Wangu” kwa ajili ya kupendezesha na kuhifadhi mazingira ya jiji hilo.

“Sisi Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania tunalo jukumu la kuanzisha na kusimamia misitu na rasilimali zake nchini, katika kumuunga mkono Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwenye upandaji wa miti, tumetoa miche 3,000 ya miti katika uzinduzi wa kampeni hiyo, na mingine 5,000 tutaitoa kwa ajili ya kupandwa wakati wa masika. Tunaomba wananchi wajitokeze kwa wingi na kutuunga mkono katika upandaji wa miti,”alisema.

Awali akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mama Salma Kikwete, Kijitonyama ambako pia alikabidhi miche mingine 600 kwa ajili ya shule hiyo, Kaimu Mtendaji Mkuu huyo aliwaasa wanafunzi kuwa mstari wa mbele kupenda mazingira, kupanda miti na kuitunza.

Pia, aliiasa jamii kwa ujumla kuacha mara moja uharibifu wa misitu kwa kuwa ni kwenda kinyume na sheria.

Naye Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Luhaga Mpina, akizungumza na waandishi wa habari alisema asilimia 61 ya nchi inakaribia kuwa jangwa kutokana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji miti kwa ajili ya mkaa na rasilimali zingine za misitu.

“Sehemu kubwa ya misitu inaharibiwa nchini jambo linalosababisha asilimia 61 ya ardhi kuwa hatarini kugeuka jangwa hivyo serikali imeamua kuchukua hatua za makusudi kunusuru hali hiyo,”alisema.

Akizungumzia hatua hizo za serikali, alisema umeandaliwa mpango wa miaka mitano wa kitaifa wa upandaji miti ambapo kila wilaya nchini imepangiwa kupanda miti 2,000,000 kwa mwaka.

Mpina alisema baadhi ya viongozi wa vijiji na halmashauri wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu kazi za upandaji miti kwenye maeneo yao, hivyo kuahidi kutembelea kila mkoa na wilaya kuona kama kweli miti inayotolewa na inapandwa ipasavyo.

“Sitakubali kuona Ilani ya UchaguziyaCCMikichakachuliwa na baadhi ya viongozi wasio waadilifu, tutafuatilia kila wilaya na mkoa kuona kama agizo hilo linatekelezwa,”alisema Mpina.

Aliongeza kuwa mpango mwingine wa serikali ni kupeleka nishati ya gesi kwenye kaya zaidi ya milioni 30 nchini ili ziondokane na matumizi ya mkaa kunusuru misitu na mazingira.

Naibu Waziri Mpina alisema mpango huo utazishirikisha wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Nishati na Madini.

Alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali katika upandaji miti kutunza mazingira na kuepuka uharibifu wa misitu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.